Saudi Arabia iliwasilisha rasmi malalamiko kwenye Umoja wa Mataifa-UN siku ya Jumatatu kuhusu kushambuliwa kwa ubalozi wake katika mji mkuu wa Iran siku ya jumamosi, baada ya Riyadh kutekeleza adhabu ya kifo dhidi ya kiongozi maarufu wa dhehebu la kishia.
Katika barua iliyopelekwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, pamoja na marais wa baraza la usalama na baraza kuu la Umoja wa Mataifa, balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa, Abdallah al-Mouallimi, alilaani vikali uvamizi kwenye ubalozi wake wa Tehran na uharibifu kwenye ofisi zake ndogo za ubalozi katika mji wa Mashhad nchini Iran.
Kwa upande mwingine katika barua yake kwa mkuu wa Umoja wa Mataifa, mwakilishi wa Iran, Gholamali Khoshroo alikiri kwamba kiasi cha waandamanaji 8,000 walifanya maandamano ya amani ambayo yalibadilika na kushindwa kudhibitika licha ya juhudi kubwa za kutuliza waandamanaji zilizofanywa na polisi. Alisema kwamba zaidi ya waandamanaji 40 walikamatwa na uchunguzi wa kuwapata wengine zaidi unaendelea.