Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 14:12

Rais Kagame akanusha kumteka Rusesabagina


Paul Kagame

Kagame hakusema wazi namna Rusesabagina alivyokamatwa, lakini alisema walimfanyia mbinu ya kwenda Rwanda kabla ya kumkamatwa

Rais Paul Kagame wa Rwanda Jumapili amekanusha kwamba serikali yake ilimteka Paul Rusesabagina ambaye sasa anashikiliwa nchini humo kwa makosa ya ugaidi na mengineyo.

Rusesabagina ni maarufu duniani kutokana na alivyoonyeshwa katika filamu ya Hotel Rwanda kama shujaa aliyesaidia kuokoa maisha ya mamia ya watu wakati wa mauaji ya halaiki nchini humo.

Katika mkutano na wanahabari kwa njia ya mtandao kutoka mji mkuu wa Rwanda, Kigali, Rais Kagame hakusema wazi namna Rusesabagina alivyokamatwa, lakini alisema kwamba walimfanyia mbinu ya kusafiri kwenda Rwanda kabla ya kukamatwa kwake.

Alisema si kweli kwamba Rusesabagina alitekwa na maafisa wa Rwanda nje ya nchi hiyo. Kigali ilitangaza kumshikilia Rusesabagina Agosti 1, na kumwonyesha kwa umma akiwa amefungwa pingu.

Kumekuwa na habari tofauti kwamba Rusesabagina alikamatwa na maafisa wa Rwanda katika uwanja mmoja wa ndege nje ya Ubelgiji ambako amekuwa akiishi kwa miaka kadhaa sasa.

Idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai ya Rwanda imeeleza kwamba Rusesabagina anakabiliwa na mashitaka kadhaa ikijumuisha ya ugaidi, kufadhili ugaidi, uhaini, utekaji na mauaji.

Rwanda imemshutumu Rusesabagina kwa kushiriki katika mashambulizi ya waasi wa National Liberation Front – FLN – kusini mwa Rwanda katika mpaka na Burundi hapo mwaka 2018.

Paul Rusesabagina ana uraia wa Ubelgiji lakini alikuwa na hati halali za kuishi Marekani hadi alipokamatwa.

Rais Kagame pia amezungumzia maandamano yaliotokea wiki iliyopita mbele ya ubalozi wa Rwanda mjini Kinshasa nchini DRC, wale waliopanga maandamano hayo walikuwa nyuma ya mpango mpana wa kuharibu uhusiano mzuri wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wiki iliyopita mbele ya ubalozi wa Rwanda mjini Kinshasa kulitokea maandamano makubwa yakishinikiza kwamba balozi wa Rwanda nchini humo Vincent Karega arejeshwe Rwanda kutokana na sababu ambazo hazikufafanuliwa. “Hivi vita ambavyo vimekuwa vikitokea vina historia yake, kupotosha ukweli kwa kurahisisha mambo huku wakisema kila kitu kinasababishwa na Rwanda, lakini hilo ni wazi na ni rahisi kulielewa, wanafanya hivi ili kupata nafasi ya kuficha nafasi yao kwenye matatizo ambayo yamekuwa yakitokea na jinsi walivyohusika kwenye matatizo hayo” alisema rais Kagame.

Kagame pia amezungumzia uhusiano wa Rwanda na mataifa ya Uganda na Burundi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni yamekuwa mahasimu wakubwa wa Rwanda “uhusiano wetu na Burundi na Uganda bado una doa kidogo bado unahitaji kazi zaidi za kufanya ili uweze kuboreka na watu waishi vyema, kwa upande wa Burundi nadhani mmekuwa mkifuatilia sisi tulifanya kila liwezakanalo ili kwenda na wakati tuliofikia,lakini ilionekana kwamba wenzetu wa Burundi ni kama hawakuitikia” aliongeza rais huyo.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG