Wakati dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya kupambana na rushwa, ripoti hizo zinaonyesha kuwa kundi la vijana linaathirika na vitendo vya rushwa na kupelekea asilimia kubwa ya vijana kukosa fursa za ajira kutokana na ajira kutolewa kwa upendeleo na hongo pamoja na kuathiri upatikanaji wa huduma bora za elimu na afya hali inayopelekea vijana wengi kukata tamaa.
Esther Thomas kijana kutoka Mwanza amesema rushwa pia imekuwa ikiwanyima vijana fursa za kugombea nafasi za uongozi kutokana na vitendo vya rushwa kushamiri kwenye vyama vya siasa hali inayopelekea vijana wenye sifa za uongozi kutokupata nafasi hizo.
“Kwenye vyama vyetu rushwa inawanyima sana vijana fursa ya kupata nafasi za uongozi, kwenye kugombania nafasi hizo vyama vyetu vingi vimeathiriwa na rushwa na inafanya vijana wenye uwezo wa uongozi ambao hawana fedha kukosa fursa na hilo ni jambo baya sana,” alisema Thomas.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya rushwa ya mwaka 2023 iliyotolewa na shirika la Transparency International, Tanzania imepata alama 40 kati ya 100 na kushika nafasi ya 87 ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 94 mwaka 2022 suala linaloonyesha Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vitendo vya rushwa.
Dkt Dotto Bulendu Mhadhiri Chuo kikuu cha Mtakatifu Agustine Mwanza amesema licha ya ripoti kuonyesha kupiga hatua lakini kumekuwa na utoaji wa huduma za kijamii usioridhisha huku ripoti za mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) za kila mwaka zimeendelea kuonyesha uwepo wa rushwa kwa kiwango kikubwa.
Amesema “inawezekana watu wakaona rushwa imepungua kwasababu kesi zilizopo katika tovuti ya taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Tanzania zimepungua”
“Lakini kiuhalisia ukiangalia utoaji wa huduma unavyofanyika na pesa ambayo imekwa pale kwa kuangalia tu ripoti za maeneo matatu ripoti ya CAG, mbio za mwenge na hata kwa macho utaona bado tunachangamoto kubwa ya rushwa”. Aliongeza.
Hata hivyo Dkt Bravious Kahyoza Mchumi na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala jijini Dar es Salaam amewataka vijana kuendelea kuelimishana na kujenga kawaida ya kupiga kelele dhidi ya vitendo vya rushwa na kuishinikiza serikali kuwachukulia hatua wale wanaokutwa na hatia ya kufanya vitendo hivyo.
“Vijana wanao wajibu wa kuelimishana utaona kwamba vijana wanalalamika kuhusu masuala ya rushwa bila kuchukua hatua za kiwango kikubwa za kutaka kuwajibika zaidi katika kuwahoji na kuvionyesha hivi vitendo na kuchukua hatua kali”
“mfano mzuri majirani zetu Kenya utaona vijana wamekuwa wakali zaidi kupitia mitandao ya kijamii kuweza kusukuma na kutaka kuwawajibisha wanaofanya vitendo hivyo” amesema.
Kauli mbiu ya siku ya Kupamba na Rushwa mwaka 2024 inasema “Kuungana na vijana Dhidi ya rushwa, kutengeneza uadilifu wa kesho” wasomi wakisisitiza umuhimu wa kufuata sheria zilizotungwa dhidi ya rushwa ili kumaliza changamoto hiyo.
Forum