Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 06:15

Ramaphosa akiri tatizo la umeme Afrika Kusini limeathiri sekta ya madini


Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akihutubia katika mkutano wa uwekezaji katika sekta ya madini Indaba, jijini Cape Town, Afrika Kusini, Febuari 7, 2023.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akihutubia katika mkutano wa uwekezaji katika sekta ya madini Indaba, jijini Cape Town, Afrika Kusini, Febuari 7, 2023.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa anasema tatizo la umeme limeathiri kwa kiwango kikubwa sekta ya madini, nguzo muhimu ya uchumi.

Ramaphosa alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia katika mkutano mkubwa wa Afrika wa uwekezaji katika madini wa Indaba.

Baraza la Madini la Afrika Kusini, ambalo linawakilisha makampuni ya uchimbaji madini, linakadiria kuwa jumla ya ujazo wa madini ulipungua kwa asilimia 6, au dola bilioni 1.8 mwaka jana.

Katika hotuba yake, Rais Cyril Ramaphosa alikiri kwamba ukatikaji wa umeme unaoendelea ulitekelezwa kwa siku 200 mwaka 2022 na kuchangia kushuka kwa madini.

“Tatizo la umeme limeleta athari kubwa katika sekta ya madini kama ilivyokuwa kwa sekta nyingine. Miezi sita iliyopita, tulitangaza mpango wa kitaifa wa utekelezaji wa nishati ili kuboresha utendaji kazi wa vituo vyetu vya umeme vilivyopo na kuongeza uwezo wa uzalishaji mpya kwenye gridi ya taifa haraka iwezekanavyo.”

Ramaphosa alisema ukweli kwamba serikali sasa inaruhusu makampuni ya madini kuzalisha umeme wao wenyewe bila vikwazo vyovyote italeta mabadiliko makubwa.

Mchumi mkuu wa baraza la madini la Afrika Kusini, Henk Langenhoven, alisema hotuba ya rais iligusa vidokezo vyote vinavyofaa kuhusu ni hatua gani inachukuliwa kutatua matatizo.

"Nadhani ukweli kwamba mgao unamgusa kila mwananchi na kila mpiga kura ni muhimu kushughulikia jambo hilo. Na hivi majuzi tumeona uharaka na msukumo kutoka kwa rais, na hazina yetu ya kitaifa ina oparesheni ya pamoja hasa kwa kuangalia hili. Na wamekuwa wakifanya kazi sana kujaribu na kuharakisha ili hatua zitekelezwe haraka iwezekanavyo."

Akigusia changamoto nyingine za usafiri na usafirishaji, Langenhoven alisema mauzo ya makaa ya mawe ambayo kwa miezi 12 yalikuwa juu kwa karibu asilimia 150 kutokana na mahitaji yaliyosababishwa na vita vya Russia dhidi ya Ukraine, pia yalipungua kutokana na vikwazo katika reli na bandari za Afrika Kusini.

Katika harakati za kutatua masuala haya, baraza litakuwa likifanya kazi na kampuni ya serikali ya uchukuzi na usafirishaji, Transnet. Ramaphosa alikaribisha ushirikiano huo katika hotuba yake, akisema sekta ya kibinafsi ni muhimu.

Mkutano wa uwekezaji wa madini wa Afrika, Indaba, unaofanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Cape Town unamalizika Alhamisi.

XS
SM
MD
LG