Maelfu ya waandamanaji wanaoipinga serikali waliandamana hivi leo Jumamosi nchini Yemen, baadhi yao wakiwa wamekasirishwa na Rais Ali Abdullah Saleh kulikataa pendekezo la yeye kujiuzulu.
Moja ya maandamano yalifanyika katika mji wa kusini wa Taiz, eneo la tukio la mapambano ya kutisha hapo jana kati ya majeshi ya usalama na waandamanaji wanaoipinga serikali. Walioshuhudia wanasema watu wanne waliuawa na dazeni kujeruhiwa katika ghasia za Ijumaa.
Waandamanaji pia waliandamana hivi leo katika mji wa bandari wa Aden.
Wakati huo huo, Yemen imemuita balozi wake aliyeko Qatar. Shirika la habari la serikali SABA limetangaza uamuzi huo hivi leo baada ya Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Hamad bin Jassem al-Thani kusema siku ya Alhamisi kwamba baraza la ushirikiano wa ghuba lenye nchi sita wanachama linatarajiwa kufikia makubaliano na Bwana Saleh ambayo yatamtaka ajiuzulu wadhifa wake. Shirika la habari la Yemen linasema balozi huyo ameitwa kwa mashauriano.
Katika muda wa miezi miwili iliyopita, waandamanaji wanaoipinga serikali wamekuwa wakitaka kumalizwa kwa utawala wa miaka 32 wa rais wa nchi hiyo. Rais Saleh ameahidi kujiuzulu, lakini baada ya uchaguzi mpya kuitishwa.
Shirika la habari la ufaransa AFP linasema vikozi vya kijeshi vya Yemen vimepiga maeneo yanayoshukiwa ni maficho ya Al Qaida kusini mwa nchi hiyo hivi leo baada ya kuwasihi wakazi wa eneo hilo kuondoka huko.
Rais Ali Abdullah Saleh alikataa pendekezo la kuachia madaraka.