Alikuwa akisumbuliwa Amyloidosis, ugonjwa adimu ambapo protini isiyo ya kawaida hujilimbikiza kwenye viungo na kusababisha kutofanya kazi vizuri.
Musharraf aliingia madarakani baada ya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu Oktoba 12, 1999, na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu aliyechaguliwa kidemokrasia Nawaz Sharif.
Aliahidi kurejesha demokrasia, Musharraf aliendelea kutawala kwa karibu miaka tisa, akishikilia ofisi za rais na mkuu wa majeshi kwa wakati mmoja kwa muda mwingi.
Miezi michache kabla ya Mapinduzi, wakiwa chini ya amri ya Musharraf, wanajeshi wa Pakistani walikuwa wameingia kwenye eneo la Kargil katika Kashmir inayotawaliwa na India. Hatua hiyo iliyopelekea majirani hao wenye silaha za nyuklia kukabiliana ana kwa ana kwenye uwanja wa mapambano ulioko mita 5,000 juu ya usawa wa bahari. Vita vya Kargil vilidumu kwa takriban miezi mitatu na vilimalizika baada ya Pakistan kuwaondoa wanajeshi wake kufuatia shinikizo la Marekani na kuyarudisha maeneo waliyokuwa wameyachukua kutoka India. India ilitaja idadi rasmi ya waliouawa katika vita hivyo kuwa 527, wakati makadirio ya hasara kwa upande wa Pakistani yanatofautiana kutoka mia chache hadi elfu chache.
Vita hivi viliharibu uhusiano kati ya jeshi na Waziri Mkuu Sharif, ambaye Oktoba 1999 kwa haraka alijaribu kuchukua nafasi ya Musharraf. Hata hivyo, jeshi lilikataa kukubali mlolongo huo mpya wa uongozi, likautwaa mji mkuu Islamabad, walikamkamata Sharif na kulivunja bunge, yote ndani ya saa chache.
Dikteta wa nne wa kijeshi wa Pakistan, Musharraf awali alifurahia umaarufu wake huku akiahidi kukabiliana na rushwa na kuongeza uwajibikaji. Uungaji mkono wake uliongezeka huku uchumi wa Pakistan ukistawi kutokana na misaada ya nje ambao nchi hiyo iliipokea kwa kuunga mkono muungano unaoongozwa na Marekani nchini Afghanistan.
Mtazamo wa Musharraf wa mrengo wa kuwa wazi na kadri na kukuza tafsiri ya wastani ya Uislam badala ya msimamo mkali wa Kiislamu ilipokelewa vizuri na watu wengi nchini Pakistan ambao walikuwa na wasiwasi na matukio ya Afghanistan na kukua kwa Taliban, kuwepo kwa al-Qaida na vita vya Marekani dhidi ya ugaidi.
Enzi zake zilishuhudia hali ya vyombo vya habari vya Pakistani ikibadilika huku serikali ikitoa leseni kwa mashirika kadhaa ya vyombo vya habari vya kibinafsi kuendesha chaneli za habari na burudani katika soko ambalo hadi wakati huo lilikuwa likimilikiwa na shirika la utangazaji la serikali, Pakistan Television Corporation (PTV).
Hata hivyo, utawala wake ulipoendelea mbele, vyama vikuu vya kisiasa viliendelea kukandamizwa, maelfu ya wapinzani wa kisiasa walikamatwa, na uhuru wa vyombo vya habari na mahakama ukazuiwa. Musharraf hatimaye alisitisha katiba mwaka 2007 kitendo ambacho alishitakiwa kuwa ni uhaini mwaka 2013 na kupewa adhabu ya kifo bila kuwepo mahakamani miaka sita baadaye. Adhabu hiyo ilitupiliwa mbali mwaka 2020.
Akiwa bado anashikilia wadhifa wa Mkuu wa Majeshi, Musharraf alitawala Pakistan kama Mtendaji Mkuu kutoka 1999 hadi 2001. Uamuzi wa serikali yake ya kijeshi kuunga mkono Marekani katika vita vya Afghanistan ulikuwa haukubaliki huku Pakistan ikikabiliwa na ongezeko la wanamgambo na ugaidi kutoka kwenye vikundi vya ndani vilivyounga mkono Taliban ya Afghanistan.
Akiongea na VOA miaka kadhaa baadaye, mwaka 2010, Musharraf alitetea uamuzi wake akisema Pakistan ingeteseka kama asingejiunga na muungano unaoongozwa na Marekani nchini Afghanistan.
"Na uamuzi huu ulikuwa kwa maslahi ya Pakistan, wacha niwaambie. Hatukufanya hivi kwa Marekani. Je, Pakistan inaihitaji Taliban na Utalibani? Waulize Wapakistani na nadhani kila mtu atasema hapana. Ndiyo maana hatukuwa na haja ya kuiunga mkono Taliban na kupigana dhidi ya muungano huo kwa niaba ya Taliban,” alisema.
Washington na Kabul hata hivyo mara nyingi ziliishutumu Pakistan kwa kutoa hifadhi na msaada kwa Taliban wa Afghanistan, shutuma ambazo Pakistan ilizikanusha rasmi.
Mwaka 2002 Musharraf aliandaa kura ya maoni ambayo iliimarisha nafasi yake kama mtu mwenye nguvu zaidi nchini humo kwa miaka mitano ijayo. Wapiga kura waliulizwa kusema 'ndiyo' ili kumweka katika nafasi ya rais na mkuu wa jeshi hadi mwaka 2007, ikiwa wanataka Pakistan kubaki kwenye njia ya mageuzi ya kiuchumi na ustawi. Matokeo ya kura ya maoni, yaliyopingwa na vyama vya siasa na mashirika ya kiraia,yalionyesha asilimia 97 walimuunga mkono Musharraf.
Lakini kufikia 2007 Musharraf alikabiliwa na wingi wa matatizo.
Jaribio lake la kumuondoa madarakani Jaji Mkuu wa Pakistan Iftikhar Muhammad Chaudhry kwa madai ya ufisadi lilisababisha vuguvugu la maandamanoya wanasheria nchini kote ambalo mara moja lilipata uungaji mkono wa vyama vikuu vya siasa nchini humo.
Wakati machafuko ya kisiasa yalipoongezeka Musharraf alikubali kujiuzulu kama mkuu wa jeshi, lakini sio kabla ya kusimamisha katiba na kuweka hali ya hatari Novemba 2007, akitaja "tishio kwa uhuru wa Pakistan". Shughuli zote za kisiasa zilipigwa marufuku, vyombo vya habari vilifungwa, na maafisa wakuu wa mahakama waliwekwa kizuizini.
Kufikia sasa, viongozi wawili wa kisiasa maarufu wa Pakistan, Nawaz Sharif na Benazir Bhutto, ambao walikuwa wametumia muda mwingi wa enzi ya Musharraf uhamishoni, waliruhusiwa kurejea chini ya mkataba wenye utata wa msamaha uliomaliza kesi za ufisadi dhidi yao.
Mauaji ya Bhutto Desemba 27, 2007, baada ya mkutano wa kisiasa huko Rawalpindi, yaliongeza masaibu ya Musharraf. Baadaye alishutumiwa kwa kutompa waziri mkuu huyo wa zamani usalama wa kutosha, na kusababisha kifo chake. Musharraf alikanusha mashtaka.
Baada ya dharura yake ya muda mfupi, Pakistan ilifanya uchaguzi wa bunge mwezi Februari 2008 ambapo chama cha Bhutto kilishinda. Akikabiliwa na mashtaka, Musharraf alijiuzulu kama rais Agosti 18, 2008, na kuondoka Pakistan mwaka uliofuata.
Azma yake ya kisiasa, hata hivyo, haikuisha. Akiwa safarini kati ya Dubai, Marekani na Uingereza alizindua chama cha All Pakistan Muslim League na akarejea mwaka wa 2013 ili kushiriki katika uchaguzi. Uungwaji mkono mdogo wa umma na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi wa kumfukuza kutokana na matendo yake ya awali ulimsukuma nje ya uwanja wa kisiasa.
Mwaka huo huo mahakama iliamuru rais huyo wa zamani na mkuu wa majeshi akamatwe kwa kuwafunga mahakimu mwaka wa 2007. Hata hivyo, wanajeshi walisimama upande wake, na kumzuia asiende jela.
Baada ya mpinzani wa Musharraf, waziri mkuu mara tatu Nawaz Sharif, kushinda uchaguzi wa mwaka 2013, serikali ilianza kesi dhidi ya Musharaff kwa madai ya uhaini mkubwa kwa kusimamisha katiba karibu miaka sita iliyopita.
Mwaka 2019, mahakama maalum ilimhukumu Musharraf na kumpa adhabu ya kifo. Uamuzi wa kutaka anyongwe hadharani ulikabiliwa na hasira na jeshi lenye nguvu na kupingwa na wengine wengi nchini Pakistan kwa lugha yake kali.
Mwaka uliofuata Mahakama Kuu ya Lahore ilitupilia mbali kesi ya uhaini na hukumu ya kifo dhidi ya Musharraf. Lakini akiandamwa na matatizo ya kisheria, tayari alikuwa ameondoka Pakistani kuelekea Dubai mwaka 2016 kwa madai ya kupata matibabu.
Musharraf alinusurika majaribio manne ya kuuawa kutoka kwa wanamgambo, matatu wakati wa utawala wake.
Ameacha mke, mtoto wa kike na kiume.
Facebook Forum