Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 22, 2024 Local time: 19:11

Rais wa zamani wa Comoros ahukumiwa kifungo cha maisha


Ahmed Abdallah Sambi rais wa zamani wa Comoros
Ahmed Abdallah Sambi rais wa zamani wa Comoros

Mahakama ya Usalama wa Kitaifa ya Comoros imempatia kifungo cha maisha rais wa zamani wa visiwa hivyo Ahmed Abdallah Sambi kwa uhalifu wa uhaini dhidi ya taifa, kwa kuuza hati za kusafiria kwa watu wasio na uraia katika nchi za Ghuba.

Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 64 alikuwa katika kizuizi cha nyumbani kwa karibu miaka mitano bila kufikishwa mahakamani hadi Jumatatu wiki iliyopita alipofikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Kesi hiyo ilifanyika kwa siku tatu tu, kukiwa na hali ya mivutano ndani ya ukumbi wa mahakama kati ya Jaji Omar Ben Ali aliyeongoza kesi hiyo na mawakili wa Sambi.
Akitangaza uamuzi Jaji Ben Ali alisema “Sambi anahukumiwa kifungo cha maisha kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kama inavyohitajika na sheria.”

“Mahakama inaamuru kutaifishwa mali zake zote na kusitishwa mafao anayopata kutoka hazina ya taifa,” alisema Ben Ali.
Sambi, alihukumiwa akiwa hayuko mahakamani baada ya kukataa kuhudhuria kesi yake. Alihudhuria kwa muda mrefu siku ya kwanza na kusema hadhani haki itatendeka.

“Korti hiyo haijaundwa kwa njia iliyo halali. Sitaki mahakama hii isikilize kesi yangu,” alisema Sambi kabla ya kususia kesi hiyo.

Sambi, aliyetawala visiwa hivyo kati ya 2006 hadi 2011, alihimiza kupitishwa sharia inayoruhusu kuuzwa kwa paspoti ya nchi kwa bei ya juu kwa maelfu ya wakazi wakiarabu wasio na uraia wa taifa lolote, wanaoishi Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Rais huyo wa zamani alituhumiwa kwa matumizi mabaya ya mapato ya mamilioni ya dola kutokana na mpango huo na awali alifunguliwa mashtaka ya ulaji rushwa.
Mwendesha mashtaka Ali Mohamed Djounaid ameiambia mahakama wiki iliyopita kwamba mpango huo ulisababisha hazina ya taifa kupoteza zaidi ya dola bilioni 1.8 ikiwa zaidi ya mapato jumla GDP, ya taifa hilo maskini la Bahari ya Hindi.

Lakini wakili wa Sambi, Jean-Gilles Halimi anasema “hakuna ushahidi” uliofikishwa mahakamani kuhusu kupotea kwa fedha hizo au kuonyesha akaunti ya benki ambayo fedha hizo zilipita ili kuweza kuwa ni uhalifu.

Mbali ya kupokonywa mali zake zote Sambi hatokuwa tena na haki ya kupiga kura wala kuwania nafasi yoyote ya umma.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo makamu wa rais wa zamani Mohamed Ali Soilihi alihukumiwa kifungo cha miaka 20 na mfanya biashara wa kifaransa mwenye asili ya Syria Bashar Kiwan alihukumiwa miaka 10 jela.

Washtakiwa wote wawili hawakuwepo mahakamani wakati wa kesi, maafisa wa usalama wa nchi hiyo wametoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwao.

XS
SM
MD
LG