Rais wa Tunisia ameamuru kuundwa kwa chombo maalum cha kusimamia janga la virusi vya corona nchini humo huku maambukizi yakiongezeka na umma ukiwa umeghadhibishwa na janga hilo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Tunisia, Rais Kais Saied alitangaza Jumatano, kuwa operesheni mpya ya kupambana na virusi itaendeshwa na idara ya afya ya jeshi ili kuhakikisha utekelezaji wa masharti ya virusi, kusimamia vifaa vya matibabu vilivyopo na kuratibu mkakati wa kitaifa wa virusi.
Saied alisimamisha bunge, alimfukuza kazi waziri mkuu na kuchukua madaraka yote ya kiutendaji mapema wiki hii baada ya maandamano ya kitaifa juu ya mzozo wa kiuchumi wa muda mrefu wa Tunisia na usimamizi wa serikali wa virusi.
Tunisia ina viwango vya juu vya vifo kutokana na virusi barani Afrika na imekabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa COVID-19 hadi sasa katika wiki za hivi karibuni, na maelfu ya visa na zaidi ya vifo 100 kila siku katika nchi ya watu milioni 11, kulingana na data kutoka serikalini na chuo kikuu cha Johns Hopkins.