Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliondoka nchini humo Jumanne kuelekea The Hague ili kuhudhuria kikao juu ya kesi inayomkabili katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu –ICC
Jumatatu bwana Kenyatta alitoa hotuba isiyo ya kawaida kwa wabunge na maseneta iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari na kwenye mtandao wa internet.
Katika hotuba hiyo bwana Kenyatta alimkabidhi madaraka ya muda Naibu Rais William Ruto ili yeye aweze kwenda Uholanzi bila kuacha pengo la madaraka.
Alisema anakwenda kwenye mahakama hiyo kama mwananchi wa 'kawaida' na kusisitiza kuwa kamwe hana hatia.
Yeye pamoja na Naibu Rais bwana Ruto wanashtakiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2007 ambapo maelfu ya wakenya waliuawa na wengine wengi kulazimika kutoroka katika nyumba zao.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 2007 rais wa zamani Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walikuwa wanagombania urais.
Bwana Kenyatta hata hivyo na mgombea mwenza wake William Ruto walichaguliwa na wakenya kuongoza taifa hilo na kuapishwa rasmi mwezi Aprili mwaka 2013.
Wote wawili wamekanusha kuhusika na ghasia hizo na wanatoa ushirikiano kwenye mahakama hiyo ya ICC.
Ni mara ya kwanza kwa rais anayehudumu madarakani kusimamishwa katika mahakama hiyo ya kimataifa. Kesi ya bwana Kenyatta itasikilizwa Jumatano.