Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 00:36

Rais wa Algeria aamuru uchunguzi kuhusu jaribio la kuhujumu serikali


Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune.
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune.

Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune ameamuru uchunguzi kufanyika kwa kile serikali inadai ni kuwepo njama za kuipindua baada ya benki kukosa pesa, misitu kuteketea moto na ukosefu wa maji.

Tebboune, ambaye alichaguliwa Desemba mwaka uliopita, amekuwa akijaribu kurejesha hali ya utulivu nchini Algeria baada ya kutokea maandamano makubwa yaliyomuondoa madarakani Abdelaziz Bouteflika.

Maafisa kadhaa waliokuwa katika serikali ya Bouteflika wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ufisadi.

Serikali ya Tebbourne inachukuwa kila hatua kuzuia kutokea maandamano kutokana na kupungua kabisa kwa mapato ya nchi kutoka kwa uuzaji wa Mafuta.

Wakaazi wa mji mkuu wa Algiers na miji mingine ya nchi, wanakumbana na hali ngumu ya maisha, wakikosa nguvu za umeme na maji kwa siku kadhaa.

Baadhi ya benki zimeshuhudia idadi kubwa ya watu wakitoa pesa zao.

Misitu kadhaa imeendelea kuteketea moto wakati huu wa msimu wa joto, jambo ambalo serikali inasema linatekelezwa maksudi.

Waziri mkuu wa Algeria Abdelaziz Djerad amesema kwamba matukio ya sasa nchini humo yanastaajabisha.

Djerald amesema kwamba “ukosefu wa maji unasababishwa maksudi” akiongezea kwamba “watu kadhaa wamekamatwa wakiwasha moto kwenye misitu ya nchi hiyo, huku wengine wakikamatwa wakiharibu vigingi vya umeme na kwamba matukio hayo yote yamepangwa kuvuruga utulivu wa nchi.”

Serikali ya Algeria inajaribu kila iwezalo kurejesha hali ya utulivu baada ya maandamano makubwa ya mwaka jana ya kudai mabadiliko ya kisiasa na hali bora ya maisha.

Maandamano yalipigwa marufuku mapema mwaka huu ili kuzuia kusambaa wa maambukizi ya virusi vya Corona.

Tebboune ameahidi kuimarisha ukuaji wa uchumi kutoka kwa mapato ya mafuta na gesi, kubuni nafasi za ajira na kusaidia watu maskini.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

XS
SM
MD
LG