Rais wa Russia Vladimir Putin ameitisha mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu wa usalama na sheria leo Jumatatu, siku moja baada ya kundi la watu kuuvamia uwanja wa ndege katika mkoa wa Dagestan baada ya ndege kutoka Tel Aviv nchini Israel kuwasili huko.
Mamia ya watu wenye hasira walikimbilia kwenye njia ya uwanja wa ndege huko Makhachkala, mji mkuu wa mkoa huo wenye Waislamu wengi hapo Jumapili jioni, wakiwatafuta abiria wa Israel, kulingana na ripoti za habari za Russia.
Wizara ya afya ya Dagestan imesema zaidi ya watu 20 wamejeruhiwa, huku wawili wakiwa katika hali mahututi. Alisema waliojeruhiwa ni pamoja na maafisa wa polisi na raia. Wizara ya mambo ya ndani imesema watu 60 wamekamatwa katika ghasia hizo. Haikubainika wazi kama mashtaka yalifunguliwa dhidi ya yeyote kati yao, lakini Kamati ya Uchunguzi ya Russia ilisema ilifungua uchunguzi wa uhalifu kwa madai ya kuandaa ghasia za umma.
Umati wa watu ulijitokeza katika uwanja wa ndege na kuizingira ndege hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Russia ya Red Wings, huku kukiwa na upinzani mdogo kutoka kwa polisi, vyombo vya habari vya Russia vimeripoti.
Forum