Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara, amesema atahakikisha haki za binaadamu zinaheshimiwa kote nchini humo. Katika mahojiano na idhaa ya Kifaransa ya Sauti ya Amerika Ijumaa bwana Ouattara alisema atawawekea vikwazo raia wa Ivory Coast wasiohesshimu haki za binaadamu. Alikanusha pia kuwa waasi wa zamani bado wanadhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo. Alijiita mpenda amani na rais wa raia wote wa Ivory Coast. Ripoti ya Amnesty International wiki hii inasema maelfu ya wakimbizi wa Ivory Coast wana khofu kubwa ya kurejea nyumbani wasishambuliwe na vikosi vinavyomwunga mkono bwana Ouattara. Rais Ouattara alizungumza na Sauti ya Amerika muda mfupi baada ya yeye na marais wengine watatu kutoka Afrika Magharibi kukutana na rais wa Marekani Barack Obama. Ouattara aliueleza mkutano huo kuwa wa maana na kwamba rais Obama alielezea furaha yake kuhusiana na kazi inayofanywa na viongozi wa Afrika. Rais huyo wa Ivory Coast pia alisema viongozi hao wameomba msaada wa kiuchumi kutoka kwa Marekani . Miongoni mwa marais waliokutana na bwana Obama Boni Yayi wa Benin , Mahamadou Issoufou wa Niger na Alpha Conde wa Guinea.
Rais wa Ivory Coast Alassane Outtara asema nchi yake itaheshimu haki za binaadamu