Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 13, 2024 Local time: 12:09

Rais Kenyatta asema marufuku ya kusafiri dhidi ya mataifa ya Afrika kutokana na Omicron hayafai


Kikao cha bunge nchini Kenya kikisubiri hotuba ya rais Uhuru Kenyatta.
Kikao cha bunge nchini Kenya kikisubiri hotuba ya rais Uhuru Kenyatta.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wakati akihutubia kikao cha pamoja cha bunge nchini humo Jumanne, ameeleza kuwa marufuku ya kusafiri dhidi ya mataifa ya Afrika kutokana na aina mpya ya virusi vya corona hayafai kwani vita dhidi ya maambukizi haviwezi kufanikishwa iwapo maeneo mengine yanatengwa. 

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wakati akihutubia kikao cha pamoja cha bunge nchini humo Jumanne, ameeleza kuwa marufuku ya kusafiri dhidi ya mataifa ya Afrika kutokana na aina mpya ya virusi vya corona Omicron hayafai kwani vita dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo haviwezi kufanikishwa iwapo maeneo mengine ya dunia yanayodhaniwa kuwa shida, yanatengwa.

Rais Kenyatta ameeleza kuwa serikali yake imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi yalioifanikishia nchi hiyo kuwa ya sita kwenye jedwali la mataifa tajiri barani Afrika kwa pato la taifa la shilingi trilioni 11.

Katika hotuba yake ya kila mwaka ya hali halisi ya taifa katika kikao cha pamoja cha bunge la kitaifa na bunge la Senate Jumanne, akiwa kwenye mwaka wa nane na muhula wa pili na wa mwisho madarakani, Rais Uhuru Kenyatta ameeleza kuwa katika utawala wake wa miaka minane, ameitoa Kenya kutoka nambari 12 kwenye jedwali la mataifa tajiri barani Afrika kwa kwa pato la taifa la shilingi trilioni 4.74 hadi nambari ya sita tajiri barani Afrika kwa pato la taifa la shilingi trilioni 11.1 katika kipindi amekuwa madarakani.

Rais Kenyatta, anaeleza kuwa katika utawala wake, Kenya inaongoza katika bara la Afrika katika uzalishaji wa nishati ya kijani, na ndiyo nchi inayoongoza barani Afrika kuunganisha umeme majumbani. Hadi sasa Bw Kenyatta anaeleza kuwa familia milioni 6.3 zina umeme mara tatu zaidi kutoka familia milioni 2.3 alipochukua hatamu za uongozi mwaka 2013.

Bw. Kenyatta, ameeleza kuwa uchumi wa Kenya ulikua kwa asilimia 0.3 katika kipindi cha 2020 licha ya changamoto ya Covid. Lakini katika robo ya pili ya 2021 ilisajili ukuaji wa kuvutia zaidi kuwahi kurekodiwa katika Pato la Taifa kwa asilimia 10.1.

Kwenye hotuba ya zaidi ya saa tatu inayogusia hali halisi ya maendeleo ya kiuchumi, muundo wa kijamii, hali ya utaifa na demokrasia, Kenyatta ameeleza kuwa Kenya sasa imepata funzo kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona na sasa inaweza kujitegemea. Amefichua kuwa kufikia Aprili, Kenya kupitia kiwanda chake cha Kenya Biovax Limited kitaanza kuzalisha chanjo kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Aidha, ameeleza kuwa Kenya imejenga maabara 95 zilizo na vifaa vya kisasa kupima sampuli na kutambua maambukizi ya virusi vya Corona kando na ilivyokuwa mwaka 2020 wakati Kenya ilikuwa na maabara moja tu ya kutambua maambukizi hayo, na sampuli zilisafirishwa kwa maabara ya Afrika Kusini. Hadi sasa anaeleza kuwa serikali imesambaza zaidi ya shilingi bilioni 257 kukinga raia wa Kenya dhidi ya athari ya virusi vya Corona.

Mnamo mwaka wa 2016, Kenyatta anaeleza kuwa serikali yake ilianzisha mfumo wa uzazi wa kulinda kina mama maarufu kama Linda Mama ambao hadi sasa umepunguza kiwango cha vifo vya uzazi kwa 43% na kuwanufaisha wanawake milioni 5.8 kote nchini Kenya.

Kwa mara ya kwanza Kenya inatengeneza silaha nyepesi na sare za kijeshi ambazo taifa lilikuwa linaagiza nje, ameeleza Bw Kenyatta.

Kenyatta anakariri kuwa kwa mara ya kwanza halmashauri ya ukusanyaji ushuru KRA imepitisha malengo yake licha ya kuwapo kwa mkwamo wa uchumi uliosababishwa na virusi vya Corona. Kra lililenga katika mwaka 2020 kukusanya shilingi ushuru wa shilingi trilioni 1.5 lakini lilikusanya kiasi cha shilingi trilioni 1.67, na hii imesaidia serikali kutekeleza miradi yenye umuhimu mkubwa kwa raia wa Kenya.

Kenyatta amestaajabikia marufuku ya kusafiri dhidi ya mataifa yalio kusini mwa Afrika kutokana na aina mpya ya virusi vya corona Omicron akisisitiza kuwa haifai kwani vita dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo haviwezi kufanikishwa iwapo maeneo mengine ya dunia yanayodhaniwa kuwa shida, yanatengwa.

Akionekana kurejelea mzozo wa miaka mingi kuhusu sehemu ya bahari hindi kati ya Kenya na Somalia, Kenyatta kwa mara nyingine, ameeleza kuwa hakuna hata siku moja kipande cha ardhi ya nchi kitaiondokea.

Hadi sasa, ameeleza kuwa serikali yake ya kwanza chini ya utawala wa ugatuzi, imesambaza zaidi ya shilingi trilioni 2.4 kwenye majimbo 47 katika kipindi cha miaka minane na kunung’unikia kutoidhinishwa kwa mchakato wa kufanyia marekebisho katiba ya Kenya, hatua ambayo ingeiwezesha serikali kusambaza kiasi cha shilingi bilioni 562 kila mwaka kutoka asilimia 15 hadi 35.

KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

XS
SM
MD
LG