Polisi mjini Mombasa nchini Kenya wametawanya maandamano yaliyopangwa na wafuasi wa upinzani katika mji huo, wakitaka kuwasilisha ujumbe katika tume ya uchaguzi IEBC na kuishinikiza ivunjwe.
Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi kutawanya umati mkubwa wa wafuasi wa CORD walioanza kukusanyika saa kumi na mbili alfajiri.
Tukio la kuwatawanya waandamanaji waliodai kukusanyika kwa amani lilianza kabla ya Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho kuwasili ili kuwahutubia wafuasi hao.
Kufuatia hali tete biashara mjini Mombasa zimefungwa kwa kuhofia usalama.
Picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha watu wengi wakiwa wamekusanyika huku polisi nao wakiwa katida doria.
Miongoni mwa viongozi waliokuwepo katika maandamano hayo mbali na gavana Joho ni pamoja na mwakilishi wa wanawake katika bunge la kitaifa Mishi Juma Mboko ambaye alipata fursa ya kuhutubia wananchi na mbunge wa Jomvu Badi Twalib.