Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Oktoba 10, 2024 Local time: 23:34

Polisi washutumiwa kuwatesa washukiwa wa Kawessi


Felix Kawessi
Felix Kawessi

Polisi nchini Uganda wanakabiliwa na shutuma za kuwatesa washukiwa wa mauaji ya aliyekuwa naibu mkuu wa polisi Andrew Kawessi, pamoja na kuwakamata watoto.

Lakini Rais Yoweri Museveni amewatetea polisi akisema washukiwa hao wanahitaji kipigo zaidi ya walichopata.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa shutuma dhidi ya polisi zinafuatia kilio cha washukiwa walipofikishwa mbele ya hakimu, wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa naibu wa mkuu wa polisi Felix Kawesi.

Washukiwa walieleza mahakama kwamba polisi wanawadhulumu kwa kuwachapa pamoja na mateso mengine, wakiwalazimisha kutoa taarifa, mateso yanayowaacha na maumivu ya mwili pamoja na vidonda vya kudumu.

Washukiwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya mjini Jinja, kituo kinachojulikana kwa kuwazuilia washukiwa wanaochukuliwa kuwa hatari kwa usalama wa nchi.

Japo polisi wanakanusha madai hayo na kuyaita porojo licha ya washukiwa kuwa na vidonda vinavyoonekana, Rais Yoweri Museveni akiwa katika mkutano wa kisiasa ametumia lugha ya kiganda na kusema kwamba iwapo washukiwa waliteswa, basi ni sawa, na kwamba wanahitaji mateso zaidi ya hayo.

Washukiwa wamemsimulia jaji wa mahakama ya Nakawa jijini Kampala jinsi wanavyodhulumiwa wakiwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya, lakini jaji akasema hana uwezo wa kutoa maamuzi kwani kesi inayowakabili ya mauaji inastahili kusikilizwa na Mahakama kuu.

Mawakili na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanashutumu polisi kwa kitendo hicho, huku wakihoji sababu inayofanya washukiwa ambao tayari wamefunguliwa mashtaka kuzuiliwa na polisi badala ya kuwekwa rumande gerezani. Washukiwa pia hawaruhusiwi kukutana na mawakili kwa sasa.

Dkt Livingstone Sewanyana ni mkuu wa shirika la kuetetea haki za kibinadamu nchini Uganda anayesema kwamba ni vigumu kwa mtu wa kawaida kujua yanayoendea katika kituo cha polisi cha nalufenya na hivyo ni vigumu kuwatambua wahusika katika mateso ya washukiwa.

“Mtu yeyote anayehusika na maswala ya haki, hastahili kuwatesa washukiwa. Kwa sababu hatuwezi kujua ni nani aliyehusika katika kuwatesa wahusika kutokana na mazingira magumu yaliyopo kuwafikia washukiwa, tumewaambia mawakili wetu kupata amri ya mahakama kuturuhusu kuwafikia washukiwa.”

Polisi pia wameitikia kwamba wamekuwa wakiwazuilia watoto 12 wa washukiwa wa mauaji hayo. Watoto hao nao wanahusishwa na mauaji ya Felix kaweesi.

Kati ya watoto hao, ni mtoto mwenye umri wa miaka miwili anayeugua ugonjwa wa kifafa. Polisi wamekuwa wakikana kuwakamata watoto hao tangu walipotoweka mwezi mmoja uliopita, na sasa, msemaji wa polisi maeneo ya Kampala Emilian Kayima amesema kwamba ni kweli wamekuwa wakiwazuilia ili kupata taarifa muhimu, lakini sasa wataachiliwa huru.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Uganda

XS
SM
MD
LG