Polisi nchini Uganda wamesema siku ya Jumapili kuwa wamemkamata mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 28 alipoingia kanisani katika mji mkuu wa Kampala akiwa na kilipuzi alichopanga kukitumia kufanya shambulizi.
Maafisa walikuwa wakiwatafuta wanaume wengine watatu pia wanaoaminika kutumwa kwenye mipango kama hiyo ya ulipuaji wa mabomu kwingineko nchini Uganda, polisi walisema.
Azma haikuwa dhahiri, lakini kundi la Islamic State (IS) lenye uhusiano na Allied Democratic Forces (ADF) hapo awali limefanya mashambulizi mabaya ya mabomu nchini Uganda.
ADF hapo awali lilikuwa kundi la waasi wa Uganda lakini lilitimuliwa zaidi ya miongo miwili iliyopita na kukimbilia katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako limekuwa ndio makao yake tangu wakati huo.
Mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Kintu Ibrahim, alikamatwa alipokuwa akikaribia kuingia katika kanisa la Pentekoste, Lubaga Miracle Centre, katika kitongoji cha Lubaga kusini mwa Kampala.
Forum