Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 04:11

Ouattara akutana moja kwa moja na Gbagbo


Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara akiwa na Laurent Gbagbo Jumanne mjini Abidjan
Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara akiwa na Laurent Gbagbo Jumanne mjini Abidjan

Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara Jumanne amekutana na hasimu wake wa kisiasa wa muda mrefu, ambaye ni rais wa zamani wa taifa hilo Laurent Gbagbo, huku wakikumbatiana, ikionekana ni hatua kubwa katika kutuliza taharuki za kisiasa kwenye taifa hilo la Afrika magharibi.

Shirika la habari la Reuters limesema kuwa Ouattara alianza kwa kumwambia Gbagbo kwamba amefurahi kumuona wakati wakikutana kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha muongo mmoja kwenye makao ya rais mjini Abidjan.

Wawili hao kwanza walikumbatiana kabla ya kuvua barakoa zao na kisha kutabasamu mbele ya kamera. Kwa zaidi ya muongo mmoja, Ivory Coast ambayo ni mzalishaji mkubwa wa cocoa imekumbwa na migogoro ya kisiasa na ghasia.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2010 hadi 2011 viliuwa zaidi ya watu 3,000 wakati viongozi hao wawili walipokuwa wakigombea utawala wa taifa hilo. Ghasia hizo zilizuka baada ya Gbagbo aliyekuwa rais kukataa kukubali kushindwa na Ouattarra kwenye uchaguzi wa Decemba 2010.

Baada ya mapigano hayo alikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uhalifu wa kivita mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai ya ICC, lakini mashtaka yalifutwa mwaka 2019. Gbagbo amesema katika mkutano wao alimsihi Ouattara kuendelea na juhudi za maridhiano pamoja na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa waliozuiliwa.

Ingawa serikali ya Ouattara iliruhusu Gbagbo kurejea nyumbani mwaka huu, bado anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 alichopewa Novemba 2019,wakati akiwa uhamishoni kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za benki kuu. Kufikia sasa serikali haijasema iwapo inapanga kumchukulia hatua au amesamehewa

XS
SM
MD
LG