Rais wa Marekani, Barack Obama amesema atatoa hotuba yake ya mwisho kuliaga taifa wiki ijayo, itakayoelezea mafanikio yake wakati wa utawala wake akiwa ikulu ya White House na atatoa mawazo yake wapi nchi inaelekea wakati rais mteule Donald Trump atakapoingia madarakani Januari 20.
Katika barua pepe aliyoituma kwa wafuasi wake Jumatatu, Obama amesema katika hotuba ya Januari 10 atakayoitoa katika mji wa makazi yake wa Chicago, "itakuwa fursa pekee kusema ahsante kwa safari hii ya ajabu, na kusherehekea namna mbali mbali ambazo zilimuwezesha kuibadilisha nchi hii kuwa bora zaidi katika miaka hii minane, na kuweza kutoa ushauri wapi tuelekee kutoka hapa tulipofikia."
Rais ambaye ana umri wa miaka 55 amesema, "taungu mwaka 2009, tumekuwa na sehemu yetu ya changamoto, na tumezikabili kwa ushujaa. Hivi ni kwasababu hatujawahi kuacha kuamini kile kinachotuongoza tangu tulipoanza -- ahadi yetu kuwa pamoja, tunaweza kubadilisha nchi hii kuwa bora."
Hotuba yake ni utamaduni wa siku nyingi wa marais wa Marekani, ulionanzishwa na George Washington mwaka 1796, wa kulihutubia taifa kabla ya kuondoka madarakani.
Facebook Forum