Rais wa Marekani Barack Obama amesema Alhamis kuwa Marekani itasimama kidete na Japan wakati nchi hiyo inakabiliana na tatizo kubwa kwenye viwanda vyake vya nuklia. Bwana Obama pia aliwahakikishia wamarekani kuwa mionzi ya sumu inayotoka kwenye viwanda vya nuklia vya Japan vilivyodhurika haitafika katika ufuo wa bahari upande wa Marekani.
Rais Obama alisema ana imani kuwa Japan itaweza kuinuka kutokana na janga hili na kujijenga upya kutokana na nguvu na nia ya raia wa Japan.
Maelfu ya watu waliaga dunia kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Ijumaa iliyopita pamoja na tsunami nchini Japan na kuna hofu kubwa juu ya uharibifu uliotokea kwenye viwanda vyake vya nyuklia katika eneo la Fukushima Daiichi.
Rais Obama pia alisema jeshi la Marekani limepeleka mamia ya watu wa kujitolea na mashirika fadhili kugawa chakula na maji huko Japan.
Jumatano usiku msemaji wa Rais Bw. Jay Carney alisema Rais Obama alifanya mazungumzo marefu kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Japan, Naoto Kan, juu ya hali nchini humo. Wiki hii Serikali ya Marekani iliwashauri raia wake huko Jpaan kukaa umbali wa kilomita 80 kutoka kiwanda cha nyuklia cha Fukushima.
Aidha rais Obama alisema viwanda vya nyuklia vya Marekani ni salama lakini ameiomba idara inayoshughulikia maswala ya usalama wa viwanda hivyo kufanya ukaguzi mpya kuhakikisha usalama wa hali ya juu.
Alhamis pia Rais Obama alifanya ziara ya kushtukiza katika ubalozi wa Japan hapa Washington DC na kutia saini kitabu cha risala za rambirambi.