Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kuzungumza Jumanne mjini Dallas katika jimbo la Texas kwenye kumbukumbu ya maafisa polisi watano waliouwawa wiki iliyopita katika shambulizi moja lililofanywa na mlenga shabaha.
Hii itakuwa mara ya 11 katika muda wake wa urais ambapo anahutubia jamii kufuatia ufyatuaji risasi holela. Msemaji wa White House, Josh Earnest alisema jumatatu kwamba rais atawapa pole sio tu watu wa Dallas wanaoomboleza lakini taifa zima la Marekani.
Zaidi ya watu 1,000 walihudhuria maombolezo kwa kuwasha mishumaa siku ya Jumatatu mjini Dallas mahala ambapo mkuu wa polisi mjini humo, David Brown aliwalinganisha maafisa hao waliofariki na mashujaa. Brown alisema idara ya polisi Dallas muda wote inalenga kukamilisha kazi zao na kwamba kazi zao hivi sasa ni kusaidia familia kufahamu namna ya kukabiliana na tukio hili la kuhuzunisha.
Katika shambulizi hili la wiki iliyopita pia maafisa polisi tisa wengine walijeruhiwa pamoja na raia wawili.