Rais Barack Obama wa Marekani amehutubia baraza la pamoja la bunge la Uingereza leo ambalo lilijumuisha wajumbe kutoka House of Commons na House of Lords mjini London.
Amekuwa rais wa kwanza wa Marekani kupata fursa ya kuzungumza mbele ya mabaraza yote mawili kwa pamoja na akatoa wito wa kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili ambao alisema ni "uhusiano wenye mafanikio makubwa kuliko yote katika historia ya dunia."
Obama alisema uhusiano wa Marekani na Uingereza unatokana na thamini na imani ambazo zimeunganisha watu wa nchi hizo mbili kwa miaka kadha.
Alizungumzia pia harakati zinazoendelea mashariki ya kati na kusema Marekani na Uingereza ziko pamoja katika "kuunga mkono usalama wa Israel na uhalali wa taifa la Kipalestina."