Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:48

Nitamuunga mkono Rais Samia ikiwa atakubali nchi inahitaji uponyaji- Lissu


Tundu Lissu
Tundu Lissu

Makamu mwenyekiti wa chama cha Chadema nchini Tanzania Tundu Lissu anayeishi uhamishoni Ubelgiji ameeleza azma yake ya kurudi nchini Tanzania wakati wowote.

Lissu alisema hayo katika mahojiano maalum na VOA baada ya kukutana na rais wa Tanzania Samia suluhu mjini Brussels Jumanne.

Akizungumzia dai lake la kutaka kesi ya mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe ifutwe, Lissu amesema jambo hilo sio kuingilia uhuru wa Mahakama na kwamba kesi hiyo “haina maslahi yoyote na afanye kama alivyofanya kuhusiana na kesi ya mashekhe wa Uamsho wa Zanzibar ambao walifutiwa mashitaka baada ya kukaa gerezani miaka 9 hakuna cha kuingilia mhimili wowote hapa”

Akisisitiza kwamba hajamwambia rais aongee na jaji bali mwendesha mashitaka ambaye ni mteule wa rais na anafanya kazi kama sehemu ya utawala sio sehemu ya Mahakama.

Pia kiongozi huyo wa upinzani na mgombea urais mwaka 2020 amemwambia rais kuhusu suala la serikali kutaka kuwafukuza kwa nguvu wananchi wa wilaya ya Ngorongoro kutoka eneo la mamlaka ya hifadhi kuwa ni jambo la hatari na linaweza kuchafua nchi na akasema rais amemwambia amelizuia.

Lissu pia amegusia uhuru wa vyama vya siasa kufanya kazi akisema amemweleza Rais Samia kuhusu zuio aliloliita haramu la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano na madai ya hitaji la katiba mpya nchini humo na mfumo mpya wa uchaguzi.

Itakumbukuwa mbunge huyo wa zamani na mgombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020 alinusurika katika shambulizi baya la risasi na watu wasiojulikana mwaka 2017 na amemtaka rais ahakikishe anatendewa haki kwa mambo ambayo alinyimwa baada ya shambulizi hilo, mwaka 2019 alivuliwa ubunge na mpaka sasa gari yake iko mikononi mwa Polisi.

Akizungumzia kuhusu sakata la Spika wa bunge Dr.Tulia Ackson juu ya wabunge wa Chadema amemwambia rais kwamba spika Ackson asiwafundishe Chadema namna ya kuendesha chama chao yeye anatakiwa afanyie kazi maamuzi ya chama kama wanavyompa taarifa na walishamwambia hao si wabunge wa Chadema na yeye kuwaambia mpaka mchakato ukamilike “hayo hayamhusu kabisa spika huyo na hata kama haujakamilika hawa sio wanachama wa Chadema na kwa maana hiyo kama sio wanachama wa Chadema hawatakiwi kuwa bungeni hata kwa siku moja zaidi” alisisitiza Lissu.

Lissu amesema rais Samia amewamwambia amemsikia na atayafanyia kazi hayo madai yake.

Lissu pia amesema kuna mazuri yananayofanywa na utawala wa rais Samia, akisema hasa kurejesha uhusiano na mataifa ya nje na kurejesha mapambano dhidi ya Covid lakini angependa kuona mengi zaidi kama kubadilisha sheria na taratibu ambazo zimeumiza watu wengi nchini humo.

Lakini anasema kwa ujumla hali ya jumla imebadilika tangu aingie madarakani lakini hali hiyo peke haitoshi. Lakini atamuuunga mkono ikiwa atakubali kwamba nchi inahitaji uponyaji aiongoze kuiponya nchi hiyo aliongeza.

XS
SM
MD
LG