Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 15:55

Serikali ya Nigeria yawatafuta wafuasi wa Boko Haram


Moja ya majengo yaliyoshambuliwa huko Damatura, Nigeria na kundi la Boko Haram na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 69
Moja ya majengo yaliyoshambuliwa huko Damatura, Nigeria na kundi la Boko Haram na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 69

Serikali ya Rais Goodluck Jonathan inawatafuta wanachama wa Boko Haram ambao wamekuwa wakifanya mifululizo ya mabomu na mauaji nchini Nigeria

Mivutano ni mikubwa nchini Nigeria ambako maafisa wa usalama wanawasaka wanachama wa kundi lenye itikadi kali linalodhaniwa kufanya wimbi kubwa la mashambulizi ya ulipuaji mabomu kote kaskazini ya nchi katika siku za hivi karibuni.

Maafisa wa usalama wanaamini kuwa kundi la Boko Haram lilipanga mashambulizi hayo yaliyouwa zaidi ya watu 100 tangu Ijumaa katika miji midogo yaa kaskazini na kulenga vituo vya polisi, makanisa na kambi ndogo ya kijeshi karibu na mji wa Maiduguri.

Kundi hilo lilidai kuhusika kwa bomu la mwezi Agasti dhidi ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu Abuja.

Kundi la Boko Haram ambalo lina maana kwamba “elimu ya magharibi ni haramu”, linasema linapambana kutaka kusimika sheria kali za kiislamu kaskazini mwa Nigeria. Kundi hilo linadai kwamba haliitambui serikali ya Nigeria au katiba wala mamlaka ya Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Godluck Jonathan aliteuwa kamati moja kuchunguza ghasia hizo. Kamati hiyo ilipendekeza kuanza mazungumzo na Boko Haram, lakini tu baada ya kusitisha ghasia zote na kusalimisha silaha zao. Boko Haram limekataa mazungumzo ya awali yaliyopendekezwa kwa sababu ya kile wanachosema Kuimarishwa majeshi katika majimbo ya kaskazini.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya nchi za Kiislamu- OIC - Ekmeleddin Ihsanoglu, alilaani vikali ghasia hizo Jumatatu. Mkuu huyo wa IOC yenye nchi wanachama 57 alielezea kuwa matukio ya mashambulizi ya mabomu ni vitendo vya uhalifu kinyume na thamini za kibinadamu na uislamu.

Ubalozi wa Marekani nchini Nigeria umeonya kuwa dhehebu hilo linapanga kushambulia mahoteli na maeneo mengine katika mji mkuu Abuja, wakati wa sherehe za Eid el Hajj. Maeneo hayo ni pamoja na yale ambayo yanatembelewa mara kwa mara na wanadiplomasia, wanasiasa na wageni.

Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Nigeria, Shehu Sani ameandika kuhusu Boko Haram na amewahoji viongozi wengi wa cheo cha juu wa kundi hilo anasema, utumiaji nguvu kupita kiasi unaofanywa na serikali dhidi ya kundi linasababisha wanachama kupata nguvu na kuungana zaidi.

Sani anasema serikali hivi sasa lazima ifahamu kwamba kulishughulikia Boko Haram kama kitisho cha usalama pekee hakitamaliza ghasia.

XS
SM
MD
LG