Polisi nchini Nigeria wanasema wamewakamata watu sita wenye uhusiano na kundi la ki-Islam lenye msimamo mkali walioshukiwa kufanya mashambulizi kwenye ofisi moja ya uchaguzi na kanisa moja mwanzoni mwa mwaka huu.
Idara ya usalama nchini Nigeria ilisema Jumanne kwamba watu hao wanauhusiano na kundi la Boko Haram, ambalo maafisa nchini humo wanadai kundi hilo limehusika na dazeni ya mashambulizi ya mabomu na ufyatuaji risasi kote nchini.
Idara ya usalama inasema watu sita wanashtakiwa kwa mashambulizi mawili ya mabomu huko Suleija, mji mmoja karibu na mji mkuu, Abuja. Bomu la kwanza lilitokea kwenye ofisi moja ya uchaguzi hapo April 8, wakati wa mkesha wa upigaji kura katika uchaguzi mkuu. Watu wasiopungua wanane waliuwawa. Shambulizi la bomu kanisani lilitokea Julai 10, na liliwauwa watu watatu.
Maafisa wa usalama pia walisema jumanne waligundua kiwanda kimoja kinachotengeneza mabomu karibu na Suleija. Polisi nchini Nigeria hawakusema kama watu hao sita walishukiwa kushiriki katika shambulizi la bomu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Abuja mwezi uliopita. Kundi la Boko Haram lilidai kuhusika na shambulizi hilo ambalo liliwauwa watu 23.
Serikali ya Nigeria imekuwa chini ya shinikizo la kusitisha wimbi la mashambulizi ya mabomu na mauaji ambayo yalidaiwa au yanadaiwa kufanywa na kundi la Boko Haram.
Kundi hilo lenye msimamo mkali linataka kuwepo kwa mfumo unaofuata sheria kali ya ki-Islam katika nchi hiyo yenye idadi ya wakazi wengi barani Afrika. Kundi hilo katika lugha ya ki-Hausa linamaanisha elimu ya magharibi ni haramu.
Polisi nchini Nigeria imewakamata watu sita wenye uhusiano na kundi la ki-Islam lenye msimamo mkali la Boko Haram