Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 09, 2024 Local time: 01:13

Netanyahu kuhutubia bunge la Marekani wakati vifaru vya Israel vikiendelea na oparesheni Gaza


Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akihutubia bunge la Marekani March 3 2015
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akihutubia bunge la Marekani March 3 2015

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kuomba msaada zaidi kwa Israel kuendelea kupambana na wanamgambo wa Hamas, wakati atakapohutubia mabaraza mawili ya bunge la Marekani leo Jumatano.

Ziara ya Netanyahu hapa Marekani inajiri wakati kuna shinkizo ndani ya Israel, kutaka serikali yake kuhakikisha kwamba mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza wanaachiliwa huru.

Kuna hali ya sintofahamu pia kuhusu hali ya baadaye ya Israel wakati Marekani, ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel, inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu mwezi Novemba mwaka huu.

Marekani, Misri na Qatar zimekuwa zikitafuta makubaliano ya Amani kati ya Israel na Hamas kwa muda wa miezi kadhaa sasa, ili kusitisha vita, kuachiliwa mateka na kuongeza msaada wa kibinadamu kwa watu wa Gaza.

Juhudi hizo hazijafanikiwa hadi sasa kupata suluhu huku mapigano yakiendelea Gaza na kutishia kutokea mgogoro mkubwa wa kikanda, mashambulizi yakitokea kati ya Israel na Lebanon huku wapiganaji wa Yemen wa Kihouthi wakishambulia meli za kusafirisha mizigo katika bahari ya shamu.

Wakati huo huo, raia wa Palestina wamekuwa wakihama kutoka mashariki mwa Khan Younis, kusini mwa ukanda wa Gaza huku vifaru vya Israel vikiingia sehemu hiyo baada ya Israel kuwataka wakaazi kuhama.

Vifaru vya kijeshi vya Israel vimeingia mtaa wa Bani Suhaila mjini Khan Younis, na katika wilaya zinazozunguka mji huo, vikistahimili mashambulizi kwa siku ya pili mfululizo, na kulazimisha maelfu ya raia kukimbia makwao.

Israel imesema kwamba oparesheni yake ya kijeshi, ambayo ni sehemu ya mashambulizi kadhaa kote Gaza katika wiki za hivi karibuni, inalenga kuzuia wanamgambo wa Hamas kujipanga tena.

Kulingana na maafisa wa afya wa Gaza, mashambulizi ya jeshi la Israel ya tangu jumapili wiki hii, yamesababisha vifo vya wapalestina 80 katika Khan Younis, na kujumulisha idadi ya vifo kuwa zaidi ya watu 39,000 katika muda wa miezi 10 ya mapigano.

Forum

XS
SM
MD
LG