Zaidi ya nchi 30 ikiwemo Marekani zimesema zinatambua baraza la waasi la mpito la Libya, zikitangaza kuwa kiongozi wa nchi hiyo Moammar Gadhafi hana uhalali wa mamlaka dhidi ya taifa hilo la Afrika kaskazini.
Nchi za magharibi zenye nguvu duniani zilitoa tangazo hilo ijumaa huko Instanbul wakati viongozi wake wakikutana kujadili mikakati ya kuimarisha kundi la upinzani katika juhudi zake za kumtimua bwana Gadhafi katika utawala wake wa miaka 42.
Katika hotuba yake iliyotangazwa kwa maelfu ya wafuasi wake kwenye mji wa Zlitan bwana Gadhafi alikanusha utambuzi huo wa kidiplomasia . Alitoa wito kwa wafuasi wake kupuuzia maelezo hayo ya kidiplomasia akisema kuwa hayana msingi.
Nchi kadhaa zenye nguvu duniani tayari zimewatambua waasi. Marekani na washirika wake watatoa msaada kwa waasi kama sehemu ya mali za Libya walizozizuiya miezi michache iliyopita ikiwemo zaidi ya dola bilioni 30 zilizokuwemo kwenye mabenki ya marekani.