Waziri wa mambo ya nje wa Marekani amesema Alhamisi kuwa wanajeshi watiifu kwa kiongozi wa Libya Moammar Ghadafi wamerudi nyuma baada ya siku tano za mashambulizi ya angani kutoka kwa majeshi ya ushirika, lakini wangali kitisho kwa raia.
Bi Clinton pia alikaribisha uamuzi wa NATO kuchukua jukumu la kuongoza majeshi hayo ya ushirika na kuhimiza azmio la Umoja wa mataifa la marufuku ya ndege nchini humo.
Mwandishi wa VOA David Gollust anaripoti kutoka wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuwa waziri Clinton alitoa tamko hilo kufuatia uamuzi wa NATO katika mkutano wa Brussels kuchukua uongozi wa majeshi ya ushirika kutoka kwa Marekani.
Hata hivyo Clinton alitahadharisha kuwa ingawa majeshi ya Ghadafi yameweza kurudi nyuma kutoka maeneo ya waasi katika mji wa Benghazi na kwingine, bado ni tishio kubwa kwa usalama wa raia wa Libya.
Alisema katika siku zijazo, baada ya NATO kuchukua uongozi wa majeshi ya ushirika, kipaumbele kitakuwa kulinda raia. Operesheni hii tayari imeokoa maisha lakini hatari ingalipo. Na ikiwa Ghadafi bado anaendelea kutishia maisha ya raia wake na kukiuka maagizo ya Umoja wa Mataifa, ni sharti jamii ya kimataifa iwe macho na makini.
Waziri Clinton pia alisema mchango wa nchi za kiarabu ni muhimu, na kukaribisha hatua ya utawala wa United Arab Emirates (UAE )ya kutoa ndege zake 12 kuhimiza azmio la Umoja wa mataifa linalozuia ndege za Libya kutumika kushambulia raia na waasi,na hivyo kuungana na wenzao wa Qatar.
Utawala wa Obama ulikuwa umeeleza nia ya kuondoka kwenye uongozi wa majeshi hayo ya ushirika lakini kubaki katika operesheni hiyo.
Aidha Clinton alisema mashambulizi ya majeshi ya ushirika yamefanikiwa kuzuia majeshi ya angani na ya ulinzi ya Ghadafi kurusha ndege zao kufanya mashambulizi.
Uturuki ambayo ni mshirika mkuu wa NATO miongoni mwa nchi za Kiislam ilisisitiza umuhimu wa majeshi ya NATO kuchukua tahadhari inapofanya mashambulizi ya angani kuzuia maafa kwa raia wa Libya.