Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 06:29

Raila akubali kutafuta haki mahakama kuu Kenya


Raila Odinga akiwataka wafuasi wake kugoma kwenda kazini siku ya Jumatatu, Agosti 13, 2017
Raila Odinga akiwataka wafuasi wake kugoma kwenda kazini siku ya Jumatatu, Agosti 13, 2017

Muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, siku ya Jumatano ulitangaza kuelekea katika mahakama ya juu kutaka uamuzi wa IEBC kumtangaza Uhuru Kenyatta Rais wa Kenya kubatilishwa.

Hili linatokea wiki moja baada ya Wakenya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa 2017 na kuwachagua viongozi wa nyadhifa mbalimbali za uwakilishi.

Rais Kenyatta alitangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo kuwa rais kwa muhula wa pili baada ya kunyakuwa ushindi.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA amesema Raila Odinga ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Kenyatta katika uchaguzi huo anaeleza kuwa ulimwengu utafahamu yaliyojiri katika mchakato mzima wa upigaji kura.

Hatua hii ya upinzani inajiri siku chache baada ya kuwepo vurugu za kisiasa katika baadhi mitaa ya mabanda vyungani mwa jiji kuu la Nairobi pamoja na mji wa Kisumu ambapo pamekuwapo na tuhuma kuwa maafisa wa kulinda usalama wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji.

Ghasia hizo zilitokana na madai ya wapinzani kutoridhishwa na hatua ya tume ya uchaguzi kumtangaza Kenyatta kuwa madarakani kwa awamu ya pili.

IEBC ilimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi katika kinyang’anyiro cha urais kwa kujizolea kura milioni 8.2 kwa asilimia 54 dhidi ya Odinga aliyemfuata kwa kura milioni 6.7 ikiwa ni asilimia 44.

Japo upinzani hapo awali ulikuwa umetangaza kuwa hutaelekea mahakamani, ni rasmi sasa viongozi hawa wa upinzani wamebadili msimamo wao.

Na kando na kusisitiza kuwa uamuzi wao kwenda mahakamani umetokana na hatua ya serikali kupitia mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya kuratibu mashirika yasiyo ya serikali kusimamisha na kudhibiti shughuli za mashirika yanayotetea haki za kibinadamu Kenya Human Rights Commission pamoja Africa Centre for Open Governance.

Taasisi hizo zinatuhumiwa kukwepa kulipa ushuru na kuendesha shughuli zao bila hati zinazostahili, Odinga anaeleza kuwa hii itakuwa nafasi bora mno kwa wakenya na ulimwengu kufahamu yaliyoenda mrama katika mchakato mzima wa kura.

Aidha, Odinga anasisitiza kuwa ushindi wa Kenyatta unatokana na shughuli za kompyuta zilizoelekezwa na maafisa wa uchaguzi. Na hivyo basi ili kuhakikisha kuwa kila mkenya anajivunia haki yake ya kidemokrasia, Odinga anaeleza kuwa mahakama ya juu imepewa nafasi nyingine kutoa uamuzi unaoafiki matakwa ya wakenya wote.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, upinzani unatakiwa kuweka maombi rasmi ya kupinga matokeo ya kura ya urais siku saba baada ya tume ya uchaguzi kutangaza mshindi wa kura hiyo. Siku mbili za mlalamishi kumkabidhi mshitakiwa hati za ulalamishi kuhusu ombi hilo, siku nne za mlalamishi kuikabidhi mahakama ushahidi. Siku nane baad ya mahakama kupokea hati hizo, itasikiliza pande husika katika kesi hiyo na kufanya uamuzi chini ya kipindi cha siku kumi na nne.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG