Mwendesha mashitaka wa Burundi Valentin Bagorikunda, amewasilisha ripoti ya uchunguzi uliofanywa na mahakama kuhusu maandamano yaliotishwa mwishoni mwa mwezi Aprili na jaribio la kuipinduwa serikali lililofanywa tarehe 13 Mei mwaka huu.Kulingana na ripoti hiyo, bilioni 52 sarafu za Burundi sawa na dola milioni 28 ndio gharama ya hasara iliyopatikana kufuatia maandamano hayo ya kushinikiza rais Pierre Nkurunziza asigombee wadhifa kwa muhula wa tatu.
Licha ya hayo, alishindia kiti hicho katika uchaguzi uliokosolewa na jamuiya ya kimataifa. Ripoti hiyo inasema mauwaji ya askari jeshi na wananchi yalitekelezwa katika maandamano hayo ambayo hayakuwa halali lakini haijagusia mauwaji ya wandamanaji yaliyofanywa na polisi wakati wakuzima maandamano hayo.
Ripoti hiyo inasema kuwa baadhi ya walioitisha maandamano hayo ni pamoja na wajumbe wa mashirika ya kiraiya yaliojikusanya na kuundaa uasi maarufu kama ‘hakuna muhula wa tatu kwa rais Nkurunziza’. Vile vile inalaumu baadhi ya vyombo vya habari, vyama vya upinzani pamoja na watu binafsi.
Bw Bagorikunda amesema pesa zilikusanywa kutoka kwa watu binafsi pamoja na wafanyabiashara kadhaa ili kuwapa wandamanaji chakula, madawa ya kulevya na tairi zilizokuwa zikichomwa wa maandamano hayo. Kwenye mkutano na wandishi wa habari mapema leo, ameongeza kuwa walioitisha mandamano walikuwa na uhusiano na kundi la askali jeshi waliojaribu kupinduwa serikali tarehe .
Amedai kuwa wana ushahidi wa kutosha kuwa vyombo vya habari na baadhi ya wandishi wa habari walishirikishwa kwenye harakati za jaribio la mapinduzi ya kijeshi na kuitisha mandamano. Amesema kuwa uchunguzi utakapomalizika, wote waliohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.