Mgombea wa Muslim Brotherhood Mohamed Morsi ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa duru ya pili ya urais nchini Misri.
Umati mkubwa ulikuwa ukishangilia kwenye eneo la Tahrir Square ambako wafuasi wa bwana Morsi walikusanyika hivi leo.
Sherehe za umati huo hivi leo zilikuwa tofauti baada na karibu mwaka mmoja na nusu uliopita wakati wananchi wa Misri walipojazana katika eneo hilo wakati wa maandamano ambayo yaliiangusha serikali ya rais Hosni Mubarak.
Tume ya uchaguzi ya Misri ilitakiwa itoe matokeo wiki iliyopita, lakini ilisema inahitaji muda zaidi kuchunguza tuhuma za ubadhirifu ambazo wagombea wote wawili waliwasilisha.
Kabla ya kutolewa tangazo la matokeo ya kura, maafisa wamepeleka majeshi zaidi ya usalama katika mitaa ya Cairo na kwenye taasisi muhimu za serikali. Hadi sasa hakuna ghasia ambazo zimeripotiwa.