Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 26, 2022 Local time: 13:09

Museveni: Nitaondoka tu iwapo kuna mtu wa maana nitakayeona naweza kumuachia Uganda.


Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye anawania muhula wa sita madarakani, amesema kwamba hajaona mtu mwenye uwezo wa kuongoza Uganda kwa sasa, na hivyo ataendelea kuwa madarakani kwa sababu wapiga kura nchini humo bado wanamhitaji kuendelea kuongoza taifa hilo.

Akihutubia viongozi wa chama chake cha National Resistance Movement (NRM) katika wilaya ya Lukungiri, ambayo ni ngome ya kisiasa ya aliyekuwa mpinzani wake mkuu mara nne Dr. Kiiza Besigye, Museveni amesema kwamba wapinzani wake ni watu wazembe wanaotaka kusukumwa kama mkokoteni.

Kati ya wapinzani wake 10 katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao 2021, ni waliokuwa makamanda muhimu wakati walipokuwa msituni katika vita vilivyomwezesha kuingia madarakani mwaka 1985.

Wagombea hao ni Lt. Gen Henry Tumukunde na aliyekuwa kamanda mkuu wa jeshi Maj. Gen. Mugisha Muntu.

Dr. Kiiza Besigye si mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, lakini anamfanyia kampeni mgombea wa chama chake cha Forum for Democratic Change Patrick Amuriat.

Besigye, Tumukunde na Muntu, wanaendelea kufanya kampeni katika sehemu kadhaa za Uganda wakimtaka Museveni kuondoka madarakani wakisema kwamba ameshindwa kutekeleza sababu kuu zilizowafanya kuingia msituni na kuanzisha vita vilivyomwezesha Museveni kuingia madarakani.

Lakini Museveni amesema kwamba wanaomkosoa walishindwa na kazi licha ya kujaribu kila mara kuwaweka katika sehemu tofauti serikalini na sasa ‘wanampigia kelele.’

“Wanajua lengo langu katika siasa lakini wanataka kunishawishi niache msimamo wangu. Wanapiga kelele kwamba nastahili kuondoka madarakani utadhani sina pa kwenda,” amesema Museveni akitumia mojawapo ya lugha zinazozungumzwa magharibi mwa Uganda.

Akiwataja watatu hao ambao walikuwa marafiki wake wa muda mrefu na mmoja alikuwa daktari wake binafsi (Dr. Kiiza Besigye), kuwa watu “wasiokuwa na maana yoyote na ambao sasa wanataka aondoke madarakani.”

Amesema kwamba "huwa nakasirika sana ninaposikia watu wakiniambia kwamba niondoke madarakani, lakini huwa najaribu sana kujizuia na kuwa mtulivu.”

“Kama ulishindwa kufanya nilichokuambia, usilete vurugu kwa kuniambia kwamba niondoke madarakani. Wapiga kura ndio wanaoamua,” amesema Museveni akiongezea kwamba “hata nikiondoka nani hao wasiokuwa na maana yoyote ambao wanataka kusukumwa kama mkokoteni wanaotaka kuongoza nchi hii. Muniache niendelee kuongoza kwa sababu raia wa Uganda wananihitaji niwepo. Nitaondoka tu iwapo kuna mtu wa maana nitakayeona naweza kumuachia Uganda. Nataka niwe na uhakika mahali naiacha Uganda”

Museveni hata hivyo ameonekana kumsifu aliyekuwa waziri mkuu Amama Mbabazi na mke wake Jackline Mbabazi akisema kwamba wanafanya vya kutosha kuimarisha kilimo cha majani ya chai.

Museveni alimfuta kazi Amama Mbabazi kutoka nafasi ya waziri mkuu, baada ya kugundua kwamba alikuwa na nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.

Mbabazi aligombea urais na kumaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yoweri Museveni na Dr. Kiiza Besigye akiwa na asilimia 1 ya kura.

Aliwasilisha kesi mahakamani ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo lakini ikatupiliwa mbali kwa ukosefu wa ushahidi kwamba kulikuwepo udanganyifu katika hesabu ya kura.

Amekuwa kimya tangu wakati huo, hadi hivi karibuni alipoanza kuonekana katika picha za ikulu ya rais akiwa na rais Museveni.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG