Kampeni za uchaguzi zikipamba moto huko Uganda kumekuwepo na ripoti za mapambano kati ya wafuasi wa serikali na Upinzani katika maeneo mbali mbali ya nchi.
Mapambano kati ya wafuasi wa Yoweri Museveni na waziri mkuu wa zamani Amama Mbabazi yametokea huko Kaskazini ambako ndio ngome ya rais baada ya vijana waliovalia fulana zenye picha za rais Museveni kuvamia mkutano na kuanza fujo.
Watu tisa wamejeruhiwa katika sakata hilo na wawili kati yao wakiwa katika wodi ya wagonjwa mahututi katika hospitali ya Ntungamo magharibi mwa Uganda baada ya vijana hao kuwashambulia wenzao kwa ngumi na mateke na fimbo.
Kwa mujibu wa Amama Mbabazi fujo hizo zimekuwa zikifanyika mara kadhaa na ameomba msaada tume ya uchaguzi lakini hajasaidiwa akisema kwamba huu ni ushindani tu, sio suala la kufa na kupona.
Msemaji wa Polisi Fred Enanga amesema uchunguzi unaendelea kuhusu mkasa huo na hivi sasa wanashikilia washukiwa wawili.
Kwingineko polisi wamefyatua risasi hewani kuwatawanya vijana wanaomuunga mkono mgombea wa urais kupitia chama cha FDC Dkt. Kiiza Besigye, waliokuwa wanataka kumchoma kijana anayedaiwa kuwa mfuasi wa chama cha NRM aliyejaribu kuingilia mkutano wake Besigye.