Asasi za kiraia kwenye mji wa Rutshuru ulioko mkoa wa Kivu Kaskazini, wanalalamikia kuzembea kwa jeshi katika kukabiliana na kundi hilo, ambalo katika siku za karibuni limechukua udhibiti wa maeneo kadhaa mkoani humo.
Kundi hilo lenye Wakongomani wengi kutoka kabila la Tutsi lilipata umaarufu 2012 baada ya kuuteka mji mkuu wa Kivu Kaskazini wa Goma kabla ya kufurushwa na jeshi.
M23 lilianza tena mashambulizi mwaka 2021 baada ya kutulia kwa miaka kadhaa. Tangu wakati huo, limeteka maeneo kadhaa yakiwemo mji muhimu wa Bunagana ulioko karibu na mpaka wa Uganda.
Kongo imekuwa ikimlaumu jirani yake Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo, madai ambayo taifa hilo linakanusha vikali.