Maafisa wa afya wa Palestina wanasema mtu mmoja ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika mapigano ya usiku wa kuamkia leo Ijumaa katika mji wa Jenin huko Ukingo wa Magharibi na jeshi la Israel.
Walioshuhudia wanasema mapambano yalitokea Alhamisi usiku wakati wanajeshi wa Israel walipoingia katika kambi ya wakimbizi ya Jenin katika uvamizi wa kufanya ukamataji. Wizara ya afya ya Palestina imesema Ijumaa kuwa kijana mmoja wa Kipalestina alifariki muda mfupi baada ya kujeruhiwa na milio ya risasi ya Israel. Wengine watatu walijeruhiwa kwa risasi.
Jeshi la Israel limesema wanajeshi walikuwa wakijaribu kumkamata mshukiwa mwanamgambo wakati ghasia zilipozuka. "Washukiwa walirusha vifaa vya milipuko na kufyatua risasi kwa vikosi vya usalama, ambavyo walijibu kwa risasi za moto," jeshi lilisema katika taarifa. Halikufafanua.
Ghasia za hivi karibuni zinafuatia miezi kadhaa ya mivutano tangu vikosi vya Israel vilipoanza msako huko Ukingo wa Magharibi mwezi Machi baada ya mfululizo wa mashambulizi mabaya ya wanamgambo nchini Israel.