Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Machi 27, 2023 Local time: 13:15

Umoja Mataifa yaomba wanajeshi waongezwe Somalia


wanajeshi kutoka Uganda

Mwakilishi wa Umoja Mataifa Augustine Mahiga, asema ongezeko la vitisho vya wanamgambo Somalia yatishia uthabiti wa eneo hilo.Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa huko Somalia Balozi Augustine Mahiga aliliambia baraza la usalama kuwa ana wasiwasi na hali mbaya ya usalama huko Somalia na uwezekano wa kuathiri eneo zima. Alisema wapiganaji wa kigeni na silaha zinaingia katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika kupitia mji wa bandari wa kusini wa Kismayo.

Alikaribisha uamuzi wa umoja wa Afrika na IGAD wa kupeleka wanajeshi elfu 2 wa ziada huko Mogadishu ili kuiwezesha AMISOM kufikia kikosi cha wanajeshi elfu 8, akisema uamuzi huo lazima utekelezwe haraka. Aliongezea kuwa taasisi hizo zitaomba kuongezwa kwa walinzi wa amani.

“Kiwango cha kitisho huko Mogadishu na kusini kati mwa Somalia kimeongezeka, kwa hiyo IGAD na umoja wa Afrika wanatarajia ongezeko la wanajeshi wapya wa AMISOM huko kufikia elfu 20 katika miezi ijayo. Baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika karibuni litawasilisha ombi kwa baraza la usalama la umoja mataifa kupata idhini ya kuongezwa idadi ya wanajeshi huko Mogadishu na maeneo mengine muhimu huko Somalia,” alisema Mahiga

Hata hivyo hakusema ni nchi gani zitachangia wanajeshi wa ziada. Hivi sasa, Uganda na Burundi ndio nchi zenye kikosi cha wanajeshi elfu 6 huko.

Mwezi Juli kundi la wanamgambo la kiislamu la Al Shabab, ambalo linadhibiti eneo kubwa la kati na kusini mwa Somalia, lilidai kuhusika na shambulizi la kujitoa mhanga kwenye mji mkuu wa Uganda , ambapo watu 70 waliuawa. Balozi wa Uganda Ruhakana Rugunda, ambaye yuko kwenye baraza la usalama, alisema nchi yake pia ina wasiwasi juu ya mmiminiko mkubwa wa wapiganaji wa kigeni nchini Somalia.

Balozi wa Marekani Susan Rice, alisema Washington inakubaliana na tathmini ya umoja mataifa kuwa hali huko Somalia ni ya hatari mno na ameitaka serikali ya mpito kufanya kazi kuondoa tofauti zao za ndani. Amesema tangu wanajeshi wa AMISOM wapelekwe huko mwaka 2007, Marekani imetoa zaidi ya dola millioni 185 za kusaidia katika masuala ya kiufundi, vifaa na mafunzo kwa wanajeshi wake na amezishawishi nchi nyingine kuongeza misaada kwa jeshi.

XS
SM
MD
LG