Kundi la wanamgambo wa Somalia Al-Shabab limepata pigo kubwa baada ya kulazimishwa kusalimu amri na kuachia udhibiti wa mji wa Baidoa, mji wa tatu kwa ukubwa ambao ndio ngome kuu ya wanamgambo hao.
Kuanguka kwa Baidoa kunafuatia shambulizi la majeshi ya tume ya Umoja wa Afrika huko Somalia (AMISOM) kulikotokea katika siku hiyo hiyo ambayo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kuongeza idadi ya vikosi hivyo kwa takriban wanajeshi 6,000.
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Susan Rice amesema kura hiyo ya siri ya baraza hilo inaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kuvunja nguvu za kigaidi na kuleta amani.
Viongozi wa wawakilishi wa zaidi ya serikali 40 wanakutana Uingereza Alhamisi kwa siku moja ya mazungumzo yenye lengo la kuanzisha serikali thabiti huko Somalia. Nchi hiyo ya Pembe ya Afrika haijawa na amani au serikali kuu kwa zaidi ya miongo miwili.