Licha ya utulivu baada ya mtafaruku mwanzoni mwa wiki, mivutano bado ipo katika mpaka wenye majeshi kati ya Ethiopia na Eritrea.
Eritrea ilidai Alhamisi iliuwa zaidi ya wanajeshi 200 wa Ethiopia na kuwajeruhi zaidi ya 300.
Taarifa ya wizara ya habari haikusema ni wanajeshi wangapi wa Eritrea waliuwawa au kujeruhiwa. Hakuna uthibitisho huru juu ya idadi iliyotolewa na Eritrea katika taarifa ya Serikali hapo jana.
Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, waziri wa habari wa Ethiopia, Getachew Reda, alisema kwamba idadi hiyo sio sahihi lakini hakuzikanusha kikamilifu. Pia alisema Ethiopia haina nia ya kuelezea tathmini yake ya uharibifu wakati wa mapambano.
Reda aliongeza kwamba mtafaruku uliofanywa na utawala huko Asmara ulisitishwa na Ethiopia ilijiandaa kulipiza kile kinachoonekana kama kutoelewana na Eritrea.