Mamia ya waokoaji wamepata miili ya watu 27 wakati wakiendelea kwa siku ya nne ya kuwatafuta watu kadhaa ambao bado hawajulikani waliko baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha maporomoko ya ardhi katika kijiji kimoja magharibi mwa India, afisa mmoja amesema Jumapili.
Watu 78 bado hawajulikani walipo tangu kutokea maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Irshalwadi Jumatano usiku katika wilaya ya Raigadh, karibu kilomita 80 kutoka Mumbai, mji mkuu wa jimbo la Maharashtra.
Nyumba 17 kati ya 48 katika kijiji hicho zilifukiwa kabisa na kifusi, au zilifukiwa kiasi, maafisa wamesema. Waokoaji mara nyingi walikuwa wakitumia vitu kama fimbo na majembe. Vifaa vizito kama vile vinavyochimba ardhini pamoja na wachimbaji hawakuweza kufika kijijini kutokana na barabara kutopitika na kuwepo matope mengi sana, alisema Deepak Avadh, afisa wa Kikosi cha Kitaifa cha Kukabiliana na Maafa.
Kikosi kingine kinachohusika na mbwa, pia kilipelekwa kutafuta manusura wowote waliokwama kwenye kifusi.
Forum