Rotunda ni chumba cha duara chenye upana wa futi 96 na nafasi kubwa iliyo na dari la duara ambalo liko katikati ya jumba la Bunge la Marekani ghorofa ya pili.
Rais Donald Trump, Spika wa Bunge la Marekani Paul Ryan na Kiongozi wa waliowengi (Warepublikan) katika Baraza la Seneti Mitch McConnell wanatarajiwa Jumatano kumuenzi “mchungaji wa Marekani,” aliyefariki wiki moja iliyopita akiwa na umri wa miaka 99.
Wanafamilia 30 watafuatana na jeneza la Graham kuja mjini Washington, ambako alikuwa ni rafiki wa maraisi wa vyama vyote viwili na kuwashauri wengine kwa miongo kadhaa.
Graham atawekwa chini ya kuba maalum Jumatano na Alhamisi, kabla ya maziko yake Ijumaa karibu na nyumbani kwake huko mjini Charlotte, Jimbo la North Carolina.
“iwapo kuna Mmarekani yoyote ambaye maisha yake na mchango wake unastahili kuenziwa kwa kupewa heshima ya mwili wake kupokewa katika Bunge la Marekani, ni Billy Graham,” Ryan amesema.
Pamoja na kuwa alikutana na kila rais kuanzia Harry Truman na kuwashauri wengi, Graham aliendelea kuchukua tahadhari juu ya masuala ya kisiasa baada ya kashfa ya Watergate. Alikuwa yuko karibu sana na Richard Nixon lakini baadae alisema kuwa alihisi kuwa anamtumia.