Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:08

Mgomo wawaathiri wagonjwa hospitali za umma Kenya


Mgomo wa wauguzi uliotokea mjini Nairobi, Disemba 8, 2016.
Mgomo wa wauguzi uliotokea mjini Nairobi, Disemba 8, 2016.

Mgomo wa wauguzi ulioanza Jumatatu nchini Kenya katika majimbo kumi na nne, umewaathiri zaidi wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali za umma

Hata baada ya Wizara ya Kazi na Wizara ya Afya kuunda jopo kazi la kutatua mgogoro huo, Muungano wa wauguzi nchini humo ungali unasisitiza kuwa hautashiriki mazungumzo ya aina yoyote yenye nia ya kusitisha mgomo huo, kwani unadai umechezewa shere na serikali vya kutosha.

Zaidi ya wauguzi elfu nane katika hospitali za umma wanaendelea kushiriki mgomo huo kutaka serikali kuu na serikali za majimbo kutekeleza mkataba wa maafikiano unaowapa wauguzi malimbikizi ya marupuru.

Serikali kuu na za majimbo zalaumiwa

Na mgogoro huu unatokana na serikali kuu na serikali za majimbo kushindwa kutoa mwongozo wa kutekeleza makubaliano ya kurejea kazini yalioafikiwa mnamo Novemba 2, 2017.

Wauguzi wanalalamika kuwa hawajalipwa malimbikizi ya marupurupu ya mishahara hata baada ya kusainiwa makubaliano ya kufanya hivyo kati yake na baraza la magavana pamoja na wizara ya Afya takriban miaka miwili iliopita.

Ilani ya mgomo huo ilitolewa Disemba mwaka 2018 kama shurutisho kwa serikali na majimbo husika kama onyo la kuchelewesha malipo na kama njia ya kuipa seirkali kuu na majimbo hayo nafasi ya kuharakisha utekelezwaji wa makubaliano ya pamoja ya malipo kati ya pande husika lakini yabainika kuwa ni majimbo matatu tu yaliotekeleza mfumo huo wa ulipaji; Mombasa, Machakos na Migori.

Nini kilichokuwa katika makubaliano

Katika muwafaka uliowekwa sahihi, katika awamu ya kwanza ya utekelezwaji wa makubaliano ya kurejea kazini, wauguzi wa hospitali za umma wangeongezwa shilingi elfu tatu na vile vile kiasi hicho kupanda hadi shilingi elfu tatu mia tano kwenye awamu ya pili na ya tatu kwenye maafikiano yaliowekwa.

Sasa imeonekana kuwa ada kila mwaka katika sekta ya afya nchini Kenya, wauguzi, matabibu na madaktari Kenya kulumbana na serikali dhidi ya shutma za kushindwa kutekeleza makubaliano ya mkataba wa pamoja.

Mgomo huu unafanyika awamu kwaawamu, Jumatatu hii ukiathiri utoaji wa huduma za afya katika majimbo yafuatayo Embu, Mandera, Wajir, Homa Bay, Murang’a, Kwale, Kirinyaga, Marsabit.

Majimbo mengine yatakayo athirika

Majimbo mengine ambayo usitishwaji wa huduma za afya utafanyika ni Pokot Magharibi, Kisumu, Nairobi, Kisii, Taita-Taveta, Nyandarua, Trans Nzoia, Elgeyo Marakwet, Nyeri na Kitui. Mengine yaliosalia yamepewa muda wa kutekeleza makubaliano hayo la sivyo kitumbua kitaingia mchangani.

Hata hivyo, serikali kuu kupitia Wizara ya Kazi kwa ushirikiano na Wizara ya Afya imebuni jopokazi la kuendeleza maridhiano yenye lengo la kufuta mvutano huu na kuweka muwafaka na baadaye kuwasilisha mapendekezo katika kipindi cha siku thelathini. Waziri wa Leba Ukur Yattani ameandaa kikao mapema Jumatatu lakini wawakilishi wa muungano wa wauguzi hawakuhudhuria. Hilo likionekana kumtia hamaki Waziri Yattani.

Mwaka wa 2017, wauguzi walishiriki mgomo wa taifa na kudumu zaidi ya miezi mitano na kufuatiwa na kutiwa sahihi ya makubaliano ya kurejea kazini baada ya shughuli za utoaji huduma za matibabu kuathirika sana huku wagonjwa wengi wakitaabika zaidi na wengine kuachwa na makovu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi

XS
SM
MD
LG