Mgogoro wa kisiasa unaonekana utaongezeka zaidi nchini Libya kati ya serikali mbili hasimu, baada ya utawala mpya ulioteuliwa na bunge kumshutumu Waziri Mkuu wa sasa kwa kutumia nguvu kujaribu kuzuia utawala mpya kuapishwa.
Fathi Bashagha alitarajiwa kuapishwa mjini Tobruk, kuwa Waziri mkuu, lakini utawala wa sasa wa Tripoli unaoongozwa na Abdulhamid al-Dbeibah, umeapa kutoachia madaraka huku kukiwepo wasiwasi wa kutokea mapigano na mipasuko ya sehemu za kiutawala.
Bashagha amelalamika kwamba Dbeibah amezuia usafiri wa ndege nchini Libya ili kuzuia maafisa wa serikali mpya kusafiri hadi Tobruk na kwamba mawaziri wawili wametekwa nyara alhamisi walipojaribu kusafiri kwa kutumia magari.
Msemaji wa serikali ya Dbeibah hajatoa taarifa yoyote kuhusu madai ya kuwateka nyara mawaziri wawili, unaodaiwa kutekelezwa na wanajeshi wanaounga mkono utawala wa Dbeibah.
Kikao cha bunge cha kuapisha Bashagha kitafanyika licha ya kutokuwepo baadhi ya wanachama, ambao wanaweza kuapishwa baadaye.