Mfalme Charles wa tatu wa Uingereza alitawazwa Jumamosi huko Westminster Abbey kama ilivyokuwa kwa wafalme wengi wa nchi hiyo waliomtangulia. Mara ya mwisho kutawazwa kwa mfalme ilikuwa miaka 70 iliyopita wakati mama yake Charles, Elizabeth alipotawazwa.
Sherehe hizo za kifahari ziliongozwa na makasisi waliovalia mavazi ya kidini, sala, nyimbo za kidini zikiambatana na sauti za wavulana na wasichana wadogo waliokuwa wakiimba. Sherehe hufanyika wikiendi nzima kwa shughuli mbali-mbali zilizoandaliwa. Ingawa zinaripoti kuwa matukio kadhaa yamepunguzwa kuliko ilivyokuwa ikipangwa katika sherehe nyingine za nyuma, bado inaaminika ni sherehe zinazotumia mamilioni ya dola za walipa kodi wa Uingereza.
Charles ndiye mfalme wa kwanza kuomba dua kwa sauti ya juu wakati wa kutawazwa kwake. Baadhi ya maneno aliyotamka yanaeleza, “nijalie niwe mwenye Baraka kwa watoto wote, wa kila dini na imani, ili kwa pamoja tuweze kugundua njia za upole na kuongozwa katika njia za amani”.
Mamilioni ya watu kote ulimwenguni waliweza kushuhudia kutawazwa kwa mfalme kupitia televisheni na internet. Mojawapo ya maswali ambayo watu wengi walijiuliza ni jukumu ambalo mtoto wa kiume wa Charles, Harry angekuwa nalo katika sherehe hizo.
Harry aliingia na washiriki wengine wa familia ya kifalme na alikaa nao kwa muda mfupi kabla ya sherehe za kutawazwa kuanza.