Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 15:35

Maswala ya jumla katika uchaguzi wa Kenya


Wagombea urais wenye ushindani mkali Raila Odinga-(Kushoto) Uhuru Kenyatta (Kulia)
Wagombea urais wenye ushindani mkali Raila Odinga-(Kushoto) Uhuru Kenyatta (Kulia)

Jamii ya kimataifa inafuatilia uchaguzi mkuu wa Kenya ambao utakuwa wa kihistoria Machi 4,2013

Katika sehemu hii ya makala zetu maalum juu ya uchaguzi mkuu wa Kenya ,leo tunamulika maswala makuu ya kisiasa na kijamii,ikiwa imesalia chini ya wiki moja kabla ya Wakenya kupiga kura hiyo ya kihistoria.

Bila shaka uchaguzi mkuu ujao wa Kenya ni wa kihistoria na wa aina yake. Hii ni kutokana na viti mbalimbali vinavyogombaniwa ikilinganishwa na uchaguzi wa hapo nyuma. Lakini wapiga kura wengi mpaka hivi leo wamekanganyika kuhusiana na maswala mbali mbali. Mtihani mkubwa kabisa umo mikononi mwa tume ya uchaguzi I.E.B.C. ambayo Wakenya wanategemea haitegemea upande wowote wala kukubali vitisho vya wanasiasa au utawala uliopo katika kusimamia, kuhesabu na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo bila woga. Mchambuzi wa maswala ya kisiasa na mwanasiasa Maur Bwanamaka aansema kwa kiasi kikubwa tume ya uchaguzi I.E.B.C. inaweza kupongezwa kutokana na namna ilioyoendesha uchaguzi mdogo bila matatizo.

Hata hivyo kwa wagombea, kinyume na uchaguzi wa hapo nyuma ambapo wengi waligombea bila kujali viwango vyao vya elimu, wamejikuta katika hali ngumu kuthibitisha wana elimu. Kuna nyakati ambazo marais waliteuwa mawaziri kuiongoza wizara bila kujali ikiwa wana elimu. Kwa baadhi yao matokeo yalikuwa aibu kubwa nje ya nchi ambapo wasingeweza kujieleza wala kuonyesha uelewa wao wa wizara wanazosimamaia wakiwa kwenye mkutano na wenzao wa nchi za nje. Lakini hili sasa ni historia. Mwanaharakati wa kidemokrasia Patrick Ochieng anasema hali imebadilika na ni lazima kila mgombea athibitishe amesema na kwa wengine ni sharti wawe na shahada za digrii.

Siasa za Kenya kweli zimebadilika na kwa mujibu wa Katiba mpya waliopitisha mwaka wa 2010 mwanamke wa Kenya ana nafasi kubwa na inayotambulika kuweza kushiriki kikamilifu katika maswala ya kisiasa , kiuchumi na kijamii. Hata hivyo katika uchaguzi huu wa kihistoria, kuna wasiwasi kuwa wanawake wengi hawataweza kujitokeza kwa wingi ilivyotegemewa. Kiongozi wa kina Mama kutoka Mombasa Seraphine Tcharo anasema kina mama wengi hawakupata hamasa juu ya uchaguzi huu na nafasi yao. Na wengine hawakuwa na fedha zilizotakiwa kulipwa ili kujiandikisha kama wagombea.

Lakini sio akina Mama peke yao ambao wanaonekana kutohamasika vya kutosha kabla ya uchaguzi Mkuu wa Machi 4. Wapiga kura wenyewe wangali na maswali kuhusu ngazi mbalimbali za uchaguzi. Lakini nani atupiwe lawama kwa ukosefu wa hamasa hiyo? Mwanasiasa Bwanamaka. Anasema tume ya uchaguzi I.E.B.C. ingelifanya vyema kutoa elimu ya uchaguzi huu wa aina yake kwa umma wa Kenya.

Ifahamike kuwa bunge la Kenya sasa limepanuka na litakuwa na viti zaidi kutoka 222 hadi 290. Mchambuzi wa maswala ya kisiasa na mwanaharakati wa kidemokrasia Patrick Ochieng anasema bunge la sasa linapanuliwa, na kuna ujenzi unaendelea kwa ajili ya maseneta. Na wakati maseneta watafurahia ofisi zao mpya na kuingia kwenye kurasa za kihistoria kama maseneta kwa kwanza katika Kenya huru, majukumu yao nayo ni chungu nzima. Mwanasiasa Maur Bwanamaka anasema kazi nyingi ya maseneta itakuwa kumshauri rais. Na wanaweza pia kuwasilisha mswada wa kumwondoa madarakani endapo amekiuka sheria fulani.

Wabunge wa bunge lijalo la Kenya watakuwa na ofisi za kisasa na teknolojia ya kisasa. Pia watapewa mafunzo ya kutumia teknolojia hiyo, na Wakenya watapata fursa ya kujionea kinachofanywa na watumishi wao bungeni moja kwa moja kupitia vyombo vya habari.

Na kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutokana na kura za maoni ,kuna ushindani mkali baina ya wagombea urais wawili. Bwana Uhuru Kenyatta akiongoza kwa pointi chache akifuatiwa na waziri mkuu Raila Odinga. Hivyo mojawapo ya wasiwasi uliopo hivi sasa ni ikiwa kutakuwa na uchaguzi wa marudio. Mchambuzi Patrick Ochieng anasema wote, bwana Uhuru na Odinga wanaamini watashinda urais katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo.

Jamii ya kimataifa inafuatilia kwa karibu uchaguzi wa Kenya na viongozi wa nchi za nje wamewaasa Wakenya kufanya maamuzi yao kwa njia ya amani,kukubali matokeo na kundoa tofauti zao za kikabila. Rais wa Marekani Barack Obama ambaye babake alizaliwa Kenya aliwapelekea ujumbe wa video Wakenya akisema Marekani itashirikiana na wakenya na kuwataka kufanya maamuzi yao wenyewe na kusuluhisha tofauti zao kotini na wala sio barabarani.

Nasi hapa Sauti ya Amerika tunatumaini Wakeny watakubali matokeo ya uchaguzi huo na kudumisha amani na umoja bila kujali miegemeo yao ya kisiasa.
XS
SM
MD
LG