Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Oktoba 07, 2024 Local time: 11:04

Marekani yaunga mkono kuongezwa viti viwili vya kudumu Baraza la Usalama


Balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Linda Thomas Greenfield
Balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Linda Thomas Greenfield

Marekani inaunga mkono hatua ya kuongeza viti viwili vya kudumu kwenye baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa ajili ya mataifa ya Afrika.

Nafasi nyingine moja itatengwa kwa ajili ya mataifa madogo ya visiwani ambayo uanachama wake utakuwa wa kupokezana.

Hayo ni kulingana na balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Linda Thomas Greenfield.

Hatua hiyo inajiri wakati Marekani inatafuta kuimarisha ushirikiano wake na mataifa ya Afrika ambapo nchi nyingi hazina furaha na hatua ya Marekani kuiunga mkono Israel katika vita vya Gaza.

Marekani pia inatafuta kuimarisha ushirikiano wake na mataifa ya visiwa vya Pacific katika juhudi za kumaliza nguvu ushawishi wa China katika eneo hilo.

Thomas Greenfiled ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba tangazo lake linalenga kuleta mabadiliko katika baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa ajili ya siku za baadaye na kwamba hatua hiyo ni sehemu ya mambo ambayo rais Joe Biden angependa kukumbukwa baada ya kuondoka madarakani.

Marekani pia imekuwa ikiiunga mkono India, Japan na Ujerumani kuwa wanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Mataifa yanayoendelea yamekuwa yakishinkiza kuwa na uwakilishi kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lakini mazungumzo ya miaka mingi hayajafanikiwa.

Haijabainika iwapo uungaji mkono wa Marekani utapelekea nchi hizo kupata nafasi kwenye baraza hilo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anaunga mkono mabadiliko katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Forum

XS
SM
MD
LG