Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 06, 2023 Local time: 07:25

Marekani yatoa msaada wa dola milioni 400 kwa Burundi


Rais wa Marekani Joe Biden.
Rais wa Marekani Joe Biden.

Marekani imekubali kutoa msaada wa dola milioni 400 kwa Burundi, waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo la Afrika Mashariki amesema.

Hayo yamejiri chini ya miezi mitatu baada ya Washington kuondoa vikwazo vilivyowekewa nchi hiyo kufuatia ghasia mbaya za kisiasa na shutuma za ukiukaji wa haki za binadamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Albert Shingiro alisema kupitia ujumbe wa Twitter kwamba mpango huo unalenga kuunga mkono serikali ya Rais Evariste Ndayishimiye kwa "maendeleo endelevu."

Shingiro alisema fedha hizo zitatumika katika kuimarisha sekta za kilimo, afya, elimu, utawala bora, mazingira na sekta binafsi.

Ubalozi wa Marekani nchini Burundi ulithibitisha kwamba makubaliano ya miaka mitano "ya kuimarisha hali ya afya, misaada ya kibinadamu, kuimarisha uchumi na haki za Warundi wote" yametiwa saini.

Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Twitter, ubalozi huo haukutaja kiasi kiasi cha fedha kinachohusika.

Serikali ya Marekani mwezi Novemba ilitangaza hatua ya kuondoa vikwazo vilivyowekwa kwa Burundi miaka sita kabla, ikisifu uchaguzi, kupungua kwa ghasia na mageuzi ya Rais Ndayishimiye.

Vikwazo hivyo viliwekwa mwishoni mwa 2015 vikiwalenga maafisa wanane wa kijeshi na usalama nchini Burundi, akiwemo waziri wa usalama wa umma wakati huo Alain Guillaume Bunyoni.

Tangazo hilo limekuja siku chache baada ya Umoja wa Ulaya pia kusema kuwa utarejesha msaada wa kifedha kwa Burundi, hatua ambayo ilikosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yanasema unyanyasaji mkubwa bado unaendelea katika nchi hiyo.

XS
SM
MD
LG