Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Juni 21, 2024 Local time: 20:35

Marekani yaondoa wafanyakazi katika baadhi ya balozi


Waandamanaji nje ya ubalozi wa nchi ya magharibi Khartoum.
Waandamanaji nje ya ubalozi wa nchi ya magharibi Khartoum.
Marekani imeamrisha kuondoka kwa wafanyakazi wote wasio wa lazima na familia za wanadiplomasia katika balozi za Marekani Sudan na Tunisia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imeonya raia wa Marekani dhidi ya kusafiri katika nchi hizo kwa sababu ya kuongezeka kwa hisia mbaya dhidi ya Marekani.

Filamu iliyotengenezwa Marekani ikikashifu dini ya kiislamu ilizusha wimbi la maandamano na ghasia wiki iliyopita kote Mashariki ya Kati na maeneo mengine.

Mtu anayesemakana kuwa ametengeneza filamu hiyo binafsi Jumamosi alihojiwa na maafisa wa Marekani huko California.

Baadhi ya sehemu za ulimwengu wa kiislamu ulirejea katika hali ya utulivu Jumamosi kufuatia ghasia zilizoanza Jumanne pale Balozi wa Marekani nchini Libya Christopher Stevens alipouawa pamoja na wamarekani wengine watatu. Waandamanaji kadha wameuawa tangu wakati huo.

Tawi la kundi la al-Qaida huko Yemen limetoa wito wa ghasia zaidi dhidi ya balozi za Marekani baada ya siku kadhaa za kupinga filamu hiyo.

Polisi wa Sudan walifanya doria katika mitaa ya Khartoum Jumamosi, siku moja baada ya waandamanaji kushambulia balozi za Uingereza, Ujerumani na Marekani. Waziri wa mambo ya nje wa Sudan, Ali Karti, amegomea ombi la Marekani kupeleka wanajeshi wa Marine kulinda ubalozi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imelaani ghasia hizo na kusema ina nia ya kulinda balozi zote nchini humo.
XS
SM
MD
LG