Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Septemba 30, 2023 Local time: 22:36

Marekani yaishambulia Syria


Mtoto akilia kufuatia kile kilichoripotiwa kama shabulizi la kutumia gesi ya sumu nchini Syria.

Rais Donald Trump alitangaza Ijumaa kwamba kwa ushirikiano na Uingereza na Ufaransa, Marekani ilifanya mashambulizi dhidi yaliyolenga vituo vilivyokuwa na uhusiano na silaha za kemikali nchini Syria siku chache tu baada ya kiongozi huyo kutuma ujumbe wa Twitter ulioionya Russia "kujitayarisha kwa makombora nchini Syria."

Hatua hiyo ilijiri kufuatia tuhuma kwamba utawala wa rais Bashar al-Assad wa Syria, ulitumia gesi ya sumu kuwashambulia na kuwaua raia wake, wakiwemo watoto wachanga.

Katika hotuba yake kutoka White House Ijumaa mwendo wa saa tatu usiku saa za ukanda wa wa Mashariki mwa Marekani, Rais Trump alisema kuwa nchi hizo tatu zimeamua kuchukua hatua hiyo kama njia ya kuzima uwezekano ya mashambulizi mengine ya kutumia gesi ya sumu.

"Muda mfupi uliopita nimeamuru jeshi la Marekani kushambulia maeneo yaliyohusika na shambulizi la silaha za kemikali lililotekelezwa na utawala wa Bashar al-Assad," alisema Trump.

"Hatutakubali mashambulizi ya kemikali," aliongeza.

Trump aidha alilizishutumu Russia na Iran kwa kile alichokiita "kushirikiana na uongozi wa Syria kufanya mashambulizi kwa raia wa Syria ambayo hayakubaliki."

Na akihutubia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya kijeshi ya Marekani, Pentagon, waziri wa ulinzi Jenerali Jim Mattis alitoa maelezo zaidi kuhusu mashambulizi hayo, na kusema kuwa yalilenga vituo vitatu, kikiwemo kimoja cha utafiti na kingine cha kuhifadhi gesi ya sumu.

"Mashambulizi hayo ni makubwa zaidi ya mara mbili na yale tuliyoyafanya nchini Syria mwaka jana...na ni makubwa," alisema Mattis.

Kituo cha televisheni cha CNN kiliripoti Ijumaa usiku kwamba milipuko mikubwa ilisikika mjini Damascus punde baada ya rais Trump kutoa hotuba yake.

Katika hotuba yake, Trump aidha alieleza masikitiko yake kwamba licha ya rais wa Russia Vladmir Putin kuahidi kuchukua hatua za kuangamiza uwezo wa Syria wa kutumia silaha za kemikali, Russia bado haijafanya hivyo.

"Ni sharti Russia iamue kama itaendelea kwenye barabara hiyo au itajiunga na nchi zinazotafuta amani," alisema rais huyo.

Wakati huo huo, kituo hicho kiliripoti kwamba vikosi vya Syria vilikuwa vinakabiliana na vile vya muungano wa nchi hizo tatu kufuatia shambulizi hilo.

Habari zaidi zitafuata hivi punde...

XS
SM
MD
LG