Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 27, 2022 Local time: 11:31

Marekani iko tayari kuiondoshea vikwazo Sudan


Rais wa Sudan, Hassan al-Bashir.

Uongozi wa Obama uko katika hatua za kuondosha baadhi ya vikwazo vya fedha dhidi ya Sudan, maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani wamesema Alhamisi.

Ikulu ya Marekani inategemewa kutoa tamko hilo Ijumaa. Kulegezwa kwa vikwazo ni kufuatia hatua chanya ya serikali ya Sudan katika kupambana na ugaidi, kupunguza migogoro, na kukataa kuwahifadhi waasi wa Sudan Kusini na kurahisisha misaada ya dharura kuwafikia watu wenye matatizo.

Marekani kwanza iliiwekea vikwazo Sudan mwaka 1997, miongoni mwa vikwazo hivyo vilihusisha biashara na kuzuia rasilmali zote za serikali, kwa sababu ya malalamiko kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu na ugaidi.

Marekani iliongeza vikwazo hivyo mwaka 2006 kwa kile ilichokiita kujihusisha kwa nchi hiyo na machafuko huko Darfur.

Waziri wa Habari wa Sudan, Ahmed Bilal, ameiambia VOA kuwa wamepokea kwa furaha habari hizo za kuondolewa vikwazo kwa sababu, amesema, “zimekuwa na athari mbaya kwa nchi hiyo na watu wake.”

Amesema vikwazo viliwaongezea “matatizo wananchi” ambao hawakuwa na uwezo wa kuondoka nchini kwa ajili ya kutafuta matibabu au kuagiza teknolojia husika.

Amesema shirika la ndege la Sudan lililazimika kufungwa kwa sababu ilikuwa hakuna njia ya kupata teknolojia iliyokuwa ikipokea kutoka Marekani. Bilal amesema vikwazo hivyo havikuwa dhidi ya serikali bali vilikuwa “kinyume cha haki za binadamu.”

Maafisa wa Marekani wamesema kuwa kuondoshwa kwa vikwazo hakuna uhusiano wowote na kutajwa nchi hiyo na Marekani kuwa inadhamini ugaidi. Rais wa Sudan Omar al-Bashir anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya ya ICC.

Mwezi Septemba, Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa tamko ikiridhia ushirikiano wa Khartoum katika vita dhidi ya makundi yenye siasa kali, bila ya kutaja hatua mpya zitazofuatia au sababu ya kutolewa taarifa hiyo kwa umma.

Marekani ilisema kuwa Sudan imechukua “hatua muhimu” kwa kukabiliana na kundi la Islamic State na vikundi vya kigaidi vingine, ikiongeza kuwa Marekani itafanya kazi na nchi hiyo katika masuala ya usalama na kuendelea kuishinikiza kuheshimu haki za binadamu na demokrasia.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG