Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Juni 09, 2023 Local time: 15:00

Marekani na Israel zashtumu mahakama ya ICC


Rais wa Palestina Mahmoud Abbas

Marekani imeungana na Israel kushtumu vikali mahakama ya kimataifa inayosikiliza kesi za jinai ICC, kufuatia uamuzi wa mahakama hiyo kuanza upelelezi wa muda dhidi ya Israel juu ya uhalifu wa kivita uliofanyiwa Wapalestina.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jeff Rathke alisema ni ajabu kuona Israel ikichunguzwa na mahakama ya ICC baada ya taifa hilo la kiyahudi kustahimili maelfu ya mashambulzi ya roketi kutoka kwa magaidi dhidi ya raia wake.

Tangazo la upelelezi huo wa muda lilitolewa Ijumaa, kutathmini ikiwa kuna uhalifu unaoafiki kusikilizwa na mahakama hiyo ya kimataifa.

Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda amesema ofisi yake itafanya uchunguzi na tathmini za kibinafsi bila kuegemea upande wowote.

Rathke amesema Marekani kamwe haikubaliani na hatua ya mwendesha mashtaka wa ICC.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema uamuzi wa ICC ni ‘kashfa’ kwa sababu Utawala wa Palestina unashirikiana na Hamas, kundi la kigaidi linalofanya uhalifu wa kivita, kinyume na Israel ambayo inapambana na ugaidi na kutii sheria za Kimataifa ikizingatia mfumo binafsi wa kisheria.

Tangazo la ICC limetolewa wiki mbili baada ya Utawala wa Palestina kuwasilisha stakabadhi kadhaa kwa Umoja wa Mataifa ikiomba kujiunga na mahakama hiyo ya The Hague.

XS
SM
MD
LG