Maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa yameua watu 23 katika mji mkuu wa Cameroon Yaounde, wafanyakazi wa zima moto wamesema Jumatatu wakati wakiwatafuta waathirika zaidi.
Maporomoko ya ardhi ni ya mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua mjini Yaounde, ambako nyumba wakati mwingine hujengwa kwenye maeneo yasiyo sahihi katika milima ya jiji.
Tukio la hivi karibuni lilitokea Jumapili jioni katika wilaya ya Mbankolo, kaskazini magharibi mwa Yaounde ambako ni makazi ya watu takribani milioni tatu. Mvua kubwa ilisababisha bwawa lililokuwa limeshikilia ziwa bandia lililokuwa juu ya ardhi kupasuka, kulingana na kituo cha televisheni cha umma CRTV.
“Jana tuliwaondoa watu 15 ambao walikuwa wamefariki na asubuhi ya leo tumepata watu wanane,” afisa wa pili wa kikosi cha zima moto David Petatoa Poufong aliwaambia waandishi wa habari katika eneo hilo.
Forum